Monday, July 9, 2007

AHADI HEWA ZA CUF

WALIOCHOSHWA NA UONGO NA KUSUBIRI AHADI HEWA WAIHAMA CUF NA KUJIUNGA NA CCM PEMBA

Subira ni neno la Kiswahili lenye maana pana sana, ni kusubiri, kustahamili, kuvumilia, kungoja kwa muda mrefu sana. Lugha nyingi zimetoa methali zenye mnasaba na neno hili. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili kuna methali zisemazo “Mwenye kusubiri hajuti. Mstahamilivu Hula Mbivu. Subira yavuta kheri. Ngoja ngoja yaumiza matumbo”, ubira ni ufunguo wa peponi”.

Na katika lugha ya Kiarabu pia uko msemo ambao tafsiri yake kwa Kiswahili unasema “Hakika Mwenyezimungu yupo pamoja na wenye kusubiri”.

Pia kuna washari walioimba mmoja namkumbuka yeye alisema katika ushairi wake:-

“Nimesubiri zamani Kama ulivyonitaka
Na mengi nikajihini Ingawa na dhulumika
Kukuridhi Muhisani Hadi uliporidhika”

Mshairi huyu katika kibwagizo chake kwenye ushairi wake huu aliendelea kusema.

“Tena hakika wajua Subira ina mipaka
Watu wengi hujiua Subira ikiwatoka
Ni ngumu kuvumilia Wachache wanaovuka
Sijashindwa nnaari Japo ni ngumu subira
Nitazidi Kusubiri Sitoifanya papara”.

Hiyo ndiyo subira, stahamala na uvumilivu, na kadri nitakavyoieleza mwisho tutakuta kuwa subira, ustahamilivu na uvumilivu vyote vina mwisho. Kuna wengine utawasikia wanasema “Stahamili joto la Bekari upate Mkate”. Hebu tujiuleze! Hivi kweli binadamu anaweza kukaa kwenye tanuri la kuokea mikate kwenye bekari kwa muda wa siku ngapi asichoke? Jawabu yake kwa muda wa masaa tu ataamua kuodoka kama hajaupata mkate. Hatimaye atasema kama mateso yenyewe ni haya, ni bora kuukosa, ataamua kuusamehe.
Dhana ya subira na uvumilivu ina mashaka yake, kwani inategemea na mazingira kile unachokisubiri. Kwani wahenga wanatwambia! “Ukiisubiri iliyokwishakuiva utakula mbovu”. Na ukisubiri iliyopooza utakula iliyooza” Methali nyengine ya wahenga inasema! “Ngoja ngoja yaumiza matumbo”, kwani tumbo lenye njaa halina subira.

Tunaamini wengi wa wale wanaoamua kusubiri, huwa wana Itikadi ya Dini na wanafanya hivyo kwa kuamini kuwa kutokana na subira yao watalipwa huko Akhera siku ya hesabu. Na huwa wanasubiri tu hawalalamiki wala kunung’unika, kwani wanaamini kuwa wakifanya kinyume chake hawatapata malipo huko Akhera.

Na kuhusu uongo je?
Sisi tulipokuwa wadogo tulikatazwa sana kusema Uongo, uongo maana yake ni kusema jambo ambalo halipo si la kweli ni “Uzushi”. Ni matusi makubwa mtu mzima kuambiwa muongo. Tulipokuwa wadogo tuliambiwa kuwa adhabu ya mtu muongo kesho siku ya kiama atavutwa ulimi mpaka ufikie pima saba. Ambapo pima moja kwa vipimo vya sasa ni kama mita mbili. Halafu mtu muongo kesho Akhera atapigwa marungu ya moto. Na hatimae kuchomwa moto.

Waswahili wanasema “Muongo Muongoze” na “Njia ya Muongo ni fupi” chambilecho bibi yangu mlezi Mwana binti Hadidi siku zote alikuwa akinambia “Ukisema uongo lazima uwe na kifuniko”. Nilikuwa simuelewi alikuwa akimaanisha nini wakati ule. Kumbe maana yake, uongo wangu nisiutoe nje watu watautambua tu. Na kwa falsafa yake anamaanisha kuniambia kuwa nisiseme uongo. Kwani “Kweli itakapodhihiri uongo utajitenga tu”.

Yupo mwanafalsafa mmoja alisema “Huwezi kuwadanganya watu wote kwa wakati wote, bali utawadanganya baadhi ya watu na kwa baadhi ya wakati tu.”

Kuna matapeli wa kisiasa waliwadanganya wananchi wa Zanzibar hasa katika kisiwa cha Pemba kwa muda usiopungua miaka 15. viongozi hawa wa CUF waliwaambia watu uongo mchana, kuzimu hakuna nyota, tena uongo wao chambilecho bibi yangu ulikuwa hauna hata kifuniko.

Waliwaambia wananchi wa Pemba eti kuwa CCM haijafaanya kitu chochote cha Maendeleo tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Walisema ni bora Ukoloni wa Kisultani kuliko utawala wa CCM. Hakuna haki wala Uhuru katika nchi. Walidanganya kuwa eti ikitawala CUF bei ya kilo moja ya mchele itauzwa Tshs. 50/= , litajengwa daraja kutoka Mkoani Pemba hadi Nungwi Unguja. Eti wananchi watatoka Pemba kwenda Unguja kwa gari badala ya Boti na Meli. Almuradi waliwadanganya baadhi ya wananchi wa Pemba na wakadanganyika.

Lakini kama ilivyo kawaida kuwa, hutaweza kuwadanganya watu wote kwa wakati wote, bali utawadanganya baadhi ya watu tu, tena kwa baadhi ya wakati. Hili linathibitika kwani sio wananchi wote wapemba waliokubali kudanganywa na CUF wengine walikataa, na hao baadhi ya waliokubali kudanganywa, sasa wameanza kung’amua.

Hali hii inadhihirika kutokana na tukio lililojitokeza mwishoni mwa mwezi wa Juni mwaka huu ambapo wanachama wa CUF 54 wa kijiji cha Matungu Shehia ya Vitongoji Jimbo la Wawi Chake Chake Pemba waliamua kwa hiyari yao kuishusha bendere ya CUF katika tawi lao. Waliungoa mlingoti wa bendera wa jiti na kweka mlingoti mpya wa chuma na hatimae kupandisha bendera ya CCM, na wao wenyewe wote wakajiunga na Chama Cha Mapinduzi.

Siku ya Jumapili iliyopita tarehe 1/7/2007 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Saleh Ramadhan Ferouz alikwenda kuwakabidhi kadi za uanachama wa CCM wananchi 54 walioamua kwa hiyari yao kujiunga na Chama Cha Mapinduzi. Wakati anapokewa na mamia ya wananchi wa kijiji hicho kwa shamra shamra ya aina yake iliyoongozwa na Dufu! Mhe. Ferouz aliwauliza. Je, mmeamua kuishusha bendera ya CUF kwa hiyari yenu? Walijibu “Ndiyo kwa hiyari yetu. Na mmeamua kujiunga na CCM kwa hiyari yenu? Walijibu “Ndiyo kwa hiyari yetu. Na alizidi kuwauliza. Hamkushawishiwa na mtu yeyote? Walijibu “Ndiyo hatukushawishiwa na mtu yeyote.

Katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi. Wanachama hao walieleza sababu za kufikia uamuzi wao wa kukiacha chama cha CUF na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi. Ni kuwa wamechoka kudanganywa na viongozi wa CUF kwa kupewa ahadi hewa za kesho kesho ambazo hazitekelezeki. Aidha walisema kuwa wao wanataka maendeleo na wanaamini wakiwa ndani ya CUF hawatapata maendeleo.

Walisema, wamesubiri kwa muda wa miaka kumi na tano (15) wakiwa ndani ya CUF kijiji chao hakikupata maendeleo yoyote. Wamebakia kuwa hawana umeme, maji safi na salama, zahanati wala barabara. Lakini ndani ya siku saba tu, baada ya uamuzi wao wa kukihama cahama cha CUF na kujiunga na CCM, tayari kijiji hicho kimekwisha pata umeme na wameahidiwa kuwa Zahanati yao itamalizwa hivi karibuni, barabara na maji safi vinafuata pia.

Katika risala yao waliyoisoma katika mkutano wa hadhara mbele ya Naibu Katibu Mkuu Mhe. Saleh Ramadhan Ferouz walieleza kuwa wameamua kujenga jengo jipya lenye hadhi ya Chama ambalo litatumika kama afisi ya CCM ya Tawi lao, ambapo wenyewe wamepima kiwanja na kukusanya matufali, chokaa na mawe. Katika kuunga mkono juhudi zao, hapo hapo ulianzishwa mchango na kupatikana jumla ya Tsh 360,200/- (laki tatu na elfu sitini na mia mbili) wakati Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar yeye binafsi na familia yake amechangia T Sh 100.000/-
Mwenyekiti wa Tawi mama la CCM Ng’ambwa amechania Sh 50,000/-. Mama Shadiya Karume amechangia mifuko 25 ya saruji.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ambapo yeye alichangia Tsh 50,000/- kwa niaba ya Jimbo lake la Mpendae.

No comments: