Wednesday, July 11, 2007

VOTI KWA CCM

VOTI KWA CCM


Kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenye Munngu Mtukufu kwa kutujaalia uzima na afya njema na pia kutupa uwezo wa kutekeleza sunna muhimu ya Funga iliyokokotezwa na Mola Karima ya Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, kwa wale Waumini wa Dini ya Kiislam.

Ndugu wana CCM na wananchi kwa ujumla, kama mjuavyo, kesho ni siku ya Jumapili tarehe 30 Oktoba, 2005. Ni siku muhimu sana katika historia ya Taifa letu la Tanzania Zanzibar. Ni siku iliyopangwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, kwa lengo la kuwachagua viongozi mbali mbali wa kitaifa ikiwa ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.

Chama cha Mapinduzi kinaamini kwamba wananchi walio wengi wa Unguja na Pemba, wanauelewa mkubwa hususan masula ya kisiasa na kwamba watakuwa tayari kuitumia kikamilifu haki zao za kikatiba na kidemokrasia, jambo ambalo linatoa faraja kubwa sana kwa CCM. Kwa kuzingatia hali hiyo, sina budi kuwanasihi wana CCM na wananchi wapenda amani na utulivu wote kujitokeza kwa wingi siku hiyo na kwenda vituoni Mijini na Vijijini kwa dhamira moja tu nayo sio nyengine bali kwa ajili ya kupiga kura. Kufanya hivyo mtakuwa tayari mmetekeleza vyema haki yenu hiyo ya kuchagua viongozi mnaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2005.

Chama cha Mapinduzi kinawataka kuwatoa wasiwasi wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kuwa kuna njama na hila zilizopangwa na baadhi ya vyama vya upinzani vyenye lengo la kutaka sio tu kuwatisha wananchi na hasa wana CCM ili washindwe kwenda vituoni kupiga kura zao bali pia wanakusudia kuvuruga Uchaguzi huo na hivyo usifanyika kama ilivyokusudiwa.

Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi nachukua fursa hii kuwahakikishia wana CCM na wananchi wapenda amani wote wa Taifa hili kwamba ulinzi umeimarishwa mara dufu na hivyo hakuna mtu au kikundi cha watu kitakachopata nafasi ya kutisha watu mitaani katika siku hiyo tu ya upigaji kura bali hata baada ya shughuli hiyo nzito kukamilika. Kikubwa zaidi ni kujitokeza mapema katika vituo mlivyopangiwa na kufanya shughuli hiyo muhimu na kuwachagua viongozi mnaowataka na hasa wagombea wote wa CCM ili waweze kuendelea kuwaleta maendeleo endelevu kwa maslahi yenu na vizazi vyenu vya leo na vijavyo bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Kwa kuwa haki ya kupiga kura ni ya kila raia aliyetimiza umri na masharti yaliyowekwa na Tume ya Uchaguzi, Chama chetu cha Mapinduzi, kitaendelea na juhudi zake ikiwa ni pamoja na kuvitaka vyombo vya dola kuimarisha zaidi ulinzi ili kila raia na hasa kila mzalendo mwenye haki ya kupiga kura aweze kuitumia vyema haki yake hiyo. Hivyo, ndugu wana CCM na wananchi msikubali kubabaishwa kwa kauli za uzushi zinazotolewa na watu mitaani kwani hali ya ulinzi imeimarishwa kwa kiwango cha hali ya juu mno. Jambo la msingi ni kuamka asubuhi mapema, nenda kituoni, jipange kwenye mstari, piga kura yako kwa kuwachagua wagombea wote wa CCM kuanzia Mgombea wa Kiti cha Urais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Ukimaliza kufanya hivyo rejea nyumbani kusubiri matokeo yatakapotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na hatimaye ushangilie ushindi.

Kwa nini tunasema hivyo? Tunasema hivyo kwa sababu Chama cha Mapinduzi ndio Chama pekee chenye wanachama na wapenzi wengi zaidi kuliko Chama chengine chochote cha siasa hapa nchini. Aidha ni Chama pekee chenye nia thabiti ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kutokana na Sera zake zinazotekelezeka siku hadi siku. Sote ni mashuhuda wa jinsi gani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Amani Abeid Karume, alivyofanikiwa kusambaza kwa kiwango cha hali ya juu mno ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2000. Sina haja ya kuyataja yote yaliyopatikana. Miongoni mwake ni pamoja na :-

· Uchumi wa Taifa umekua kwa asilimia sita nukta tano (6.5%) pamoja na kusimamia vyema matumizi ya mapato.
· Miundo mbinu
Barabara mpya kwa kiwango cha lami zimejengwa Unguja na Pemba.
· Vituo vya Afya vimejengwa Mijini na Vijijini
· Umeme – umesambazwa karibu nchi nzima
· Maji safi na salama yanapatikana Mijini na Vijijini
· Serikali imefanikiwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji
· Sekta ya Elimu
i) Skuli zimeenea na mabanda yameongezeka mara dufu
ii) Vyuo Vikuu hadi kufikia vitatu
· Mawasiliano na Uchukuzi
i) Makampuni ya Simu za mkononi kama vile Zantel, Vodacom, Mobitel, Celtel n.k. zimeanzishwa na kuendelea vizuri.
ii) Usafiri wa Anga na baharini vimeimarishwa
iii) Viwanja vya ndege vya Unguja na Pemba vimepanuliwa n.k.

Kwa mantiki hiyo, wapinzani hawana uwezo wa kuishinda CCM katika Uchaguzi Mkuu huu, kwa sababu hawana Demokrasia ya kweli ndani ya vyama vyao. Hivyo, natumia fursa hii kuwaomba wana CCM na wananchi wapenda amani wote kwenda kwenye vituo vya kupigia kura kwa salama na amani. Baada ya kukamilisha kupiga kura yako, ondoka na urejee nyumbani bila ya tatizo lolote. Aidha, Chama cha Mapinduzi kinawaomba wana CCM wote kutovaa sare za Chama chetu. Hili sio ombi bali ni amri, kwani kuvaa sare kwa siku ya kupiga kura ni kosa la jinai.

UJIO WA WAANGALIZI WA KITAIFA NA KIMATAIFA:
Chama cha Mapinduzi kimefarajika na hali ya ujio wa Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Madola waliofika nchini kwa lengo la kuja kuangalia jinsi Uchaguzi huu utakavyofanyika. Aidha, nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa kumiminika kwa wingi. Lakini CCM inasema kwa kuja nchini humu kwa lengo la kuja kushuhudia jinsi gani Uchaguzi unavyofanyika na sio wamekuja kutoa maelekezo ya jinsi gani Uchaguzi huu ufanyike wala kutoa matokeo ya Uchaguzi huo.

Chama Cha Mapinduzi kinaamini kuwa kuwepo kwao kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha taarifa sahihi kwenye Jumuiya ya Kimataifa kuhusiana na hali halisi ilivyo kuanzia uwingi wa wanachama na hata wapenzi na pia jinsi gani walivyohamasika na kuwa tayari wakisubiri siku yenyewe kufika ili waweze kutumia haki zao za kidemokrasia na kuchagua viongozi wanaowataka bila ya wasiwasi wowote. Aidha, kuwepo kwao kutasaidia kubainisha ukweli na uongo wa viongozi wa vyama vya upinzani wanaojaribu kuihadaa dunia eti CCM haina wanachama na pia hawapendwi na jamii ya Wazanzibari. Kupitia mkutano wa Ufungaji wa Kampeni za CCM uliofanyika leo, tunaimani kubwa kwamba Waangalizi wameweza kujionea wenyewe hali halisi na hivyo kuweza kupima na kutambua ukweli na uongo wa vyama hivyo vya upinzani nchini.

Mwisho, kwa mara nyengine tena nachukua fursa hii kuwataka wana CCM na wananchi wapenda amani na utulivu wote wa Taifa letu, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura ili kwenda kupiga kura zenu na kukipatia ushindi wa nguvu ya tsunami Chama chenu cha Mapinduzi na hivyo kukipa ridhaa kwa mara nyengine tena ya kuongoza dola kwa miaka mingine mitano ijayo.

Ahsanteni.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.


(VUAI ALI VUAI)
KATIBU – IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI
ZANZIBAR.

No comments: