Monday, July 9, 2007

BAADA YA PROPAGANDA ZA CUF KUGONGA
MWAMBA SASA WAJIKANYAGA WENYEWE

Kuna usemi wa Kiswahili usemao “Njia ya muongo fupi” na “Muongo muongoze”.

Ndani ya kipindi kisichopungua mwezi mmoja sasa magazeti mbali mbali yamekuwa yakiandika habari zinazoelezea hisia za wana CUF kuwataka viongozi wao wajitoe katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Chama Cha Mapinduzi na Chama cha upinzani CUF. Hii inatokana na kuwa baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF kutoridhika na hali ya mazungumzo kati ya vyama hivyo yanavyoendelea.

Hapa kwanza hatuna budi kujikumbusha kwa kujiuliza suali. Nini chanzo cha mazungumzo haya ya vyama vya siasa vya CCM na CUF? Mazungumzo haya yanatokana na kile kinachoitwa mpasuko wa Kisiasa wa upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani Zanzibar.

Kama tunavyojua kuwa Zanzibar ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambao ulikuwa watatu ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa hapo tarehe 30/10/2005. Uchaguzi huu ulivishirikisha vyama vingi vya siasa, lakini kama kawaida panapo ushindani wa vyama katika uchaguzi lazima patatokea na Chama kitakachoshinda na vile vile vyama vitakavyoshindwa. Na kama matarajio yalivyotarajiwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa mshindi katika uchaguzi huo na vyama vyengine kadhaa vimeshindwa. Miongoni mwa vyama vilivyoshindwa ni Chama cha CUF. Haidhuru kimejitahidi kupata viti kiasi cha kukiwezesha kuwa ni kiongozi wa upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, lakini kama kawaida CUF imekataa kuyaheshimu matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005 jambo ambalo limekipelekea Chama hicho kutoyatambua matokeo ya Uchaguzi huo na kutomtambua Rais aliyechaguliwa katika uchaguzi huo wala Serikali yake aliyoiunda.


Pamoja na kuwa matokeo ya Uchaguzi huu yamekubaliwa na vyama vyengine vya siasa na kutambuliwa na mashirika ya Kitaifa na ya Kimataifa kadhaa yaliyokuja kuangalia mchakato mzima wa uchaguzi wenyewe. Lakini viongozi wa Chama cha CUF wamekataa kata kata kuyatambua matokeo hayo kwa madai kuwa eti uchaguzi haukuwa wa haki na huru.

Viongozi wa Chama cha CUF kama kawaida yao waliwachochea wanachama wao kwa kuwaambia uongo mwingi. Miongoni mwa mambo ya uwongo waliyowaambia wanachama wao ni kuwa Uchaguzi lazima utarudiwa au itaundwa Serikali ya Mseto au kama wanavyoiita wenyewe Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kugawana madaraka kati ya viongozi wa CCM na wa CUF kwa muda na baadae utaitishwa uchaguzi mwengine.

Pamoja na kuwa masuala haya yalikuwa yakienezwa kipropaganda lakini kwa muda wote huo Viongozi wa CUF walishindwa kwenda kwa wanachama wao kuwaeleza, mpaka pale Rais wa Jamhuri ya Muungano alipolihutubia Bunge wakati akilizindua kwa mara ya kwanza mwezi Disemba mwaka 2005 ndipo viongozi wa CUF walipopata nguvu angalau wakaweza kufanya mikutano ya hadhara. Hapo viongozi wa CUF wakatangaza bayana kuwa ili suala la Zanzibar litatuke lazima Uchaguzi urudiwe au iundwe Serikali ya Mseto (Umoja wa Kitaifa).

Kurudiwa kwa Uchaguzi wa Zanzibar na kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ndio wimbo uliokuwa ukiimbwa na viongozi wa CUF kila walipofanya mikutano yao ya hadhara. Tena waliwaambia wafuasi wao kuwa uchaguzi utarudiwa au itaundwa serikali ya mseto kabla mazungumzo hayajaanza. Ndiyo maana wanachama wa CUF waliposikia kuwa viongozi wa vyama viwili hivi wanakutana kwa mazungumzo wao walikwisha kutoa matokeo ya mazungumzo hayo kuwa ni kurudiwa kwa uchaguzi au Zanzibar kuundwa Serikali yamseto (Umoja wa Kitaifa). Na wakati mazungumzo yalipokuwa yanaendelea, tulishuhudia vombo vya habari mbali mbali hasa magazeti ya Fahamu mwananchi, Al-huda n.k. yaliandika makala kwa kuweka vichwa vya habari kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa au mseto waja Zanzibar.


Kwa sababu viongozi wa CUF walikwisha kuwambia wafuasi wao jinsi jawabu la mazungumzo kati yao na CCM litakavyokuwa, na kuwaahidi kwamba itakapofika mwisho wa mwezi wa Mei 2007 suala hili litakuwa limeshapatiwa ufumbuzi. Na kwa kuwa viongozi wao walioshiriki mazungumzo walibaini ugumu wa masuala yao ndipo sasa ulipotumika usanii wakuwaandaa baadhi ya wanachama wao kuwa wadai eti mazungumzo hayana faida na kuwataka viongozi wa Chama chao waamue kujitoa kwenye mazungumzo hayo.

Kutokana na hali hiyo ndipo zilipotoka kauli kutoka kwa wanachama wa CUF kuchoshwa na subira ya kungoja kumalizika kwa mazungumzo kwani waliona jawabu ya mazungumzo haitakuwa kama yalivyo mategemeo yao.

Kwa kuwa viongozi wa Chama cha CUF wanajua faida ya kuwepo kwa mazungumzo hayo kati ya Chama chao na Chama tawala (CCM) na athari zake za kutokuwepo kwa mazungumzo hayo kitaifa na kimataifa, sasa wameandaa usanii wa kuwaandaa wanachama wao na baadhi ya viongozi wao kuwa eti wanawashindikiza kuwa wajitoe kwenye mazungumzo na wao kujidai kuandaa vikao vyao vya Chama na kutoa uamuzi kuwa uongozi wa Chama chao umeamua kuendelea na mazungumzo.

Jambo la kushangaza viongozi hawa wa CUF tangu yaanze mazungumzo yao na Viongozi wa CCM karibuni miezi saba sasa, hawajafanya mkutano wa ndani wala wa hadhara hata mmoja kuwaelezea wanachama wao juu ya maendeleo ya mazungumzo. Leo iweje atoke kiongozi wa CCM anayeshiriki mazungumzo hayo kuja kuwaambia wanachama na wafuasi wa CUF juu ya maendeleo ya mazungumzo.

Kama wameshaona kuwa mazungumzo haya hayawaletei faida basi ni bora waamue kujitoa tu, lakini wasisingizie kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuwa amevuruga mazungumzo. Tunawambia viongozi wa CUF kama wanaona kua ni muwafaka kuwapa taarifa za mazungumzo wanachama na wafuasi wao basi wafanye hivyo. Wasitake kumtupia paka wa macho kiongozi wa CCM. Chama Cha Mapinduzi sasa kinakazi ya kuendeleza mchakato wa kupanga safu kwa kuwatafuta viongozi wake wa kukiongoza Chama kwa miaka mitano ijayo. Viongozi na Makada wake wakifanya ziara Mikoani wanakwenda kuimarisha chama chao. Msiandae shughuli kwa kutegemea wali wa matanga. Na kama mmezoea kuwambia wanachama wenu uwongo basi msiwatazamie viongozi wa CCM kuwa watakusaidieni katika hilo. Kama uongo wenu umefika mwisho basi semeni kweli.

Viongozi wa CUF katika kuendeleza usanii wao eti wanawazulia wananchi wa Zanzibar kuwa wamechoka kusubiri, na eti kuwa wamechoshwa na uongozi uliopo madarakani wakimaanisha uongozi wa Chama Cha Mapinduzi. Wakati muandishi wa makala hii alipokuwa akipita mitaani aliwakuta wananchi wa Zanzibar katika kikao chao kama kawaida jioni wakinywa kahawa aliwasikia wakisema. “Hawa CUF wamechoshwa na amani na utulivu tuliokuwa nao hapa Zanzibar, bado wanataka kuturudisha kwenye vurugu. Sisi wa Zanzibari tulishatoa uamuzi wetu kwenye visanduku tangu tarehe 30 Oktoba 2005 tunajua Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM ndiyo tuliyoichagua. CUF tuliiona na hatukuipa kura Rais tuliyemchagua ni Karume kama wao hawaridhiki basi wasubiri 2010 ili waje wamchague huyo wanayemtaka”.

Nilipowauliza juu ya suala la mazungumzo, mmoja wao alijibu “Kama ni mazungumzo na wazungumze si mazungumzo tu! Hata sisi hapa tunazungumza, usiku ukiingia tunakwenda zetu majumbani mwetu kulala”. Na juu ya Serikali ya Mseto au Umoja wa Kitaifa? Alijibu mzee mmoja wa makamo “Sisi hatutaki mseto wala Umoja wa Kitaifa kuma mseto na Umoja wa Kitaifa hapa aliuleta Karume mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari, 12, 1964 katika kuunda Serikali yake aliwashirikisha wazanzibari wa kabila na rangi zote, walikuwamo ZNP, UMMA PATI, ZPPP wa Unguja na Pemba. Sisi tunasubiri Uchaguzi Mkuu wa 2010 kama roho zikifika kama wao wanaona mbali basi na wafanye vurugu tutaona”.

Hapa tunatoa indhari kwa viongozi wa CUF kuwa, wastake kuufanya ulimwengu ukadhani kuwa wazanzibari wote ni wanchama wa CUF, Zanzibar sasa imo katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapo wanachama wa CCM, wa NCCR-Mageuzi, wa CHADEMA, wa TLP, wa JAHAZI Asilia, wa Sauti ya Umma, wa NRA nk. Ushahidi ni matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, wapo waliovipigia kura vyama hivyo nao ndio wengi kiliko waliokipigia kura chama cha CUF. Sasa wanaposema kuwa kuna watu Zanzibar wamechoshwa na uongozi wa CCM, wasiwachanganye wazanzibari wote. Waseme kuwa wana CUF tu ndio waliochoshwa na uongozi wa CCM. Hilo halina ubishi na ndio maana wakaunda Chama chao na wakakipigia kura katika chaguzi tatu mfululizo, lakini Demokrasia imewakataa. Kura walizopata hazikuwawezesha kuchaguliwa na kupewa ridhaa ya wanzanzibari kuunda serikali.

Kutokana na mambo yote tuliyoyaelea ndio maana tunasema propaganda yao imegonga mwamba sasa wanajikanyaga wenyewe, na uwongo wao sasa umefika mwisho, kwani njia ya muongo ni fupi.

No comments: