Monday, July 9, 2007

MWNYEKUPINGA NEEMA ZA MOLA II

MWENYE KUPINGA NEEMA ZA MOLA NI KAFIRI

MWAKA 2005, Watanzania tumeshuhudia nchi yetu ikifanya Uchaguzi ambao ulikuwa wa amani na utulivu, Uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza wakaguzi wa kitaifa na kimataifa walikuja kushuhudia hali halisi ya Uchaguzi huo ulivyoendeshwa. Waangalizi hao walikiri kuwa Uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki pamoja na kwamba palikuwa na kasoro ndogo ndogo (mapungufu) za hapa na pale ambazo hufanywa na kila binadamu ye yote duniani.

Pamoja na kuwa huru na wa haki, lakini pia ni Uchaguzi uliokuwa na vitendo vingi vibaya vilivyotokea wakati wa Uchaguzi wa Mwanzo na wa Pili uliohusisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa – yaani (1959 na 1963). Hapa Zanzibar, watu kubaguana kwa Itikadi zao za vyama kung’oleana mazao wanachama wa Chama fulani kuitwa Mabunju, Makafiri n.k. na haya yote yaliandaliwa na watu wanao jidai kuwa ni Masheikh, kwani hao ndio wanaojiita Masheikh na Wastaarabu na lakini kila uchao wanadiriki kutangaza Misikitini, kuwa Serikali ya Mapinduzi ni Serikali ya dhulma iliyoiondoa eti Serikali halali ya SAYYID JEMSHID BIN ABDULLAH, BIN KHALIFA BIN HAROUB, Serikali iliyokuwa ikiongozwa na MOHAMED SHAMTE BIN HAMAD.

Aidha, wanathubutu kutangaza hadharani na bila kimeme kwamba kila anayeunga mkono Chama cha Mapinduzi ni kafiri na ataingia motoni kesho huko Akhera. Kwa hali hiyo, napenda kuwauliza Masheikh hao kuwa wamezitafakari vizuri kauli zao hizo?. Wamechunguza kwa makini siri ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla?.

Nachukua nnafasi hii kuwaomba watu wa aina hiyo wayatafakari maelezo ya makala hii na hatimaye waweze kutoa maamuzi muafaka kama kweli wao ni wananchi na hasa wazalendo wa Zanzibar, kufanya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, waliyafanya kwa misingi ya haki au walifanya kwa ajili ya kutekeleza amri kua ya nani?
Siasa za kupigania Uhuru Zanzibar zilianza wakati wa utawala wa SULTAN SAYYED KHALIFA BIN HAOUB, ambaye ni babu yake Jemshid. Ni Mwarabu mwenye asili ya Oman. Kwa desturi ya Waarabu, neno kila neno linafsiri yake au linatokana na matokeo ya jambo/kitu fulani. Sasa tuangalie maana halisi ya neno SAYYED (Bwana), KHALIFA (Mtumwa), HAROUB (Matata au Vita). Ni utawala uliojaa matatizo makubwa na yasiyoweza kuvumiliwa na wananchi wowote duniani.

Hivyo, wakati wa utawala huo, Mwenye-zimungu - Mwenye Uwezo Mkubwa na Mwingi wa Rehema, aliwapa uwezo wananchi wa Visiwa hivi vya Unguja na Pemba waliokuwa wakidhalilishwa, kukandamizwa na kudharauliwa ndani ya nchi yao, ndiye aliyewafumbua macho Waafrika wa Zanzibar na kuanza kudai haki ya kujitawala. Kiongozi aliyejitolea kupigania haki hiyo si mwengine bali ni Hayati ABDEID AMANI. Kwa vile jina hilo ni la asili ya Kiarabu lina tafsirika kama ifuatavyo - ABEID (Abdi yaani Mtumishi au Mjumbe), AMANI (Utulivu). Kwa ufupi, ni majina yenye kupendelea zaidi hali ya amani na utulivu kwa mmaslahi ya wananchi wote na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa majina haya KHALIFA BIN HAROUB na ABEID AMANI KARUME, wote walikuwa ni Watawala katika nyakati tofauti, lakini tutagundua kuwa KHALIFA BIN HAROUB - Mtawala huyu alikuwa na Utawala wa Kidhalim tofauti na mwenziwe ABEDI AMANI - ni Mtumishi au Mjumbe aliyekuja kuondoa utawala wa matata/matatizo na kuweka utulivu kwa wananchi wa jamii ya Wazanzibari, waliokuwa wanayumbishwa na kubaguliwa pasipo na misingi yoyote.

Utawala wa Kisultani uliwagawa Wazanzibari, kwa misingi ya rangi, kabila, dini na jinsia na baya zaidi walitugawa wananchi kwa misingi ya Wapemba na Wazanzibari. Utawala huo uliweka pingamizi kadha dhidi ya Wapemba na Wazanzibari (Waunguja). Mathalan, Wapemba waliotaka kuja Zanzibar, walitakiwa kwanza wapate kibali kutoka kwa Sheha na Mudiri. Akifika tu Zanzibar lazima aripoti kwa Mudiri na kwa Sheha kwa nia ya kueleza ni sababu zipi za msingi zilizomfanya aje Unguja na ataishi kwa muda gani. Kwa hali hiyo, halikuwa jambo rahisi hata kidogo kwa Mpemba kuja Zanzibar ni sawa na kwenda Ulaya.

Mwaka 1954, mama yangu aliolewa Kisiwani Pemba na Bwana Juma bin Nafasi, mkaazi wa Mgelema. Namkumbuka mzee mmoja mkaazi wa Kisiwa hicho, alirejea kutoka Zanzibar. Alipokelewa na wanakijiji hicho cha Mgelema kama vile ametoka Makka, Saudi Arabia. Kina mama walikwenda kumlaki kila mmoja akiwa na mbuzi yake ya kukunia nazi ili kuweza kushiriki kikamilifu katika kukuna nazi zitakazotumika katika kuandaa chakula cha sherehe hiyo ya kumpokea mgeni huyo aliyerudi kutoka Zanzibar. Hakika, ilikuwa ni sherehe kubwa na ya aina yake. Hali hiyo ilisababishwa na utawala dhalimu wa Sultani. Utawala huo uliwafananisha Waafrika wa Zanzibar kuwa sawa na MBWA.

Nakumbuka mnamo mwaka 1953, Jemshid, mjukuu wa Sayyid Khalifa bin Haroub – mtawala wa Zanzibar (wakati huo) alimponda kijana aliyekuwa akiitwa Ali Machano, eneo la Kidongo chekundu karibu na Mental Hospital yaani Hospitali ya watu wa akili (sasa Luncastar). Jemshid bila aibu alitamka hadharani –“huyu Mbwa amechafua gari yangu”.

Sultan aliwafanya Waarabu hasa wa Oman kana kwamba ni watawala dhidi ya Waafrika. Ilifikia hadi kitendo chochote ata kachofanyiwa Muafrika na Mwarabu kina kuwa ni sawa tu. Kuna visa vingi walivyofanyiwa Waafrika, kwa mfano Mwafrika akipondwa na Mwarabu kwa baskeli, badala ya kupewa pole adabu yake anapigwa bakora na matusi juu yake yaani anaambiwa hana adabu sababu unabonde hajui wewe kama baskeli yangu kengele Lucas, Breki Nta fira Danlop sababu unabonde - yaani sababu gani amemponda kwa hivyo Mwafrika huyo hana adabu hajui kuwa Baskeli yake breki ni nta, mpira ni Danlop na kengele yake aina ya Lucas sababu amemponda hana adabu, anapigwa bakora, kupondwa kupondwa na bakora juu madam ni muafrika astahili adhabu hiyo. Wazee wetu kudhalilishwa kuchukuliwa wake zao huku wakiona, Said Sudi akiwakamata wanawake kwa nguvu mbele ya waume zao na kuwapeleka anakotaka na waume zao wakiangalia tu kwa sababu Said Soud ni katika aila ya Mfalme. Kama hiyo haitoshi, Usultani ulikuwa unawadhalilisha hata mayatima. Wakati huo nikiwa mwanafunzi wa Madrassa ya Sheikh Ameir Tajo, iliyokuwa katika mtaa wa Kwaali Nathoo, mjini Zanzibar, nilikuwa nikiwaongoza baadhi ya watoto yatima kwenda kwa Said Khalifa. Jambo la kusikitisha, kila siku tunayokwenda huko, tukifika nyumbani kwake, tulilazimishwa kupanda ngazi kwa magoti huku tukiimba “Salam Malik Rabbana Bukhlana Sultan Khalifa”. Tunapanda mpaka juu hadi kunako Seble yake (Mfalme). Hapo huja mke wake Bi. MATKA au Mfalme mwenyewe na kuanza kutoa zawadi mbali mbali zikiwemo vitambaa vya kanzu au thamani yake pamoja na wakati mwengine hupata vitambaa vya kanzu pamoja na Tshs. Tatu (3/=) kwa kila mmoja wetu na hatimaye tunarejea kwa magoti mpaka chini na kuondoka. Haya ni theluthi tu kati ya madhila kadhaa niliyoyaeleza ya Utawala ambayo mimi nimeyaona kwa macho yangu yakifanywa kwa makusudi na utawala wa Sayyid Khalifa bin Haroub.

Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba Zanzibar ni kitovu cha Uislamu na Mabingwa wa Lugha ya Kiarabu pamoja na fani ya lugha hiyo. Pamoja na maovu yote yanayofanyika hapa, hakuna hata Sheikh mmoja aliyewahi kutamka kuwa Utawala wa Sayyid Khalifa bin Haroub ni wa Kidhalimu, badala yake Masheikh hao ndio waliokaza kamba kuutetea kwa hali na mali na kutaka kuulazimisha umma wa Wazanzibari utii na umuenzi mfalme. Kwa lipi zuri hadi jamii ilazimishwe hivyo?. Hebu tumwangalie Mwana Mapinduzi Abeid Amani, baada ya kutimiza azma ya jina lake na kufaulu kuigomboa Zanzibar kutoka kwenye utawala huo wa mabavu.

Mara tu baada ya kufanikiwa Mapinduzi matukufu ya 1964, Hayati Mzee karume, aliondosha aina zote za ubaguzi, ubwana na utwana, hakujali mweusi wala mweupe, kabila au dini. Aliubadilisha Mji wa Zanzibar kuwa wa kisasa kabisa, kuboresha mfumo wa elimu hadi leo tunao Maporofesa wa Makabila na jinsia mbali mbali. Aliweza kubadili maisha ya wanyonge wote wa unguja na Pemba. Mathalan, Watumbatu wa leo sio wale wa enzi za Kiusultani waliokuwa wakitumwa kulima katika mashamba ya Mabwana wa Kiarabu, Wahindi n.k. Aidha, jamii ya Wazanzibari wa leo sio ile ya jana. Jamii ya leo inauelewa mkubwa wa mambo na kwamba wanajua hata kufanya biashara sawa na wale wa jamii ya Asia (Wahindi).

Iweje leo Masheikh “Vilemba” hao wathubutu kusema eti Utawala wa sasa una kwenda kinyume na Maadili ya Uislamu. Sina haja ya kusema chochote kuhusu hili, bali naomba kuwauliza Masheikh wa aina hiyo kwamba kila Chuo Cha Kiislamu Cha Muslim Accademy kilichokuwa na zaidi asilimia sitini (60 %) ya mashoga asilimia 60, Ule ndio uiwslamu? Nani asiyejuwa kuwa Mkamasini na Mlango wa Chuma palikuwa na Madanguro?. Jee, kuna Sheikh yeyote miongoni mwa hao tunaowazungumza aliyewahi kukanusha?.

Kama kweli wanapenda haki basi hawana budi kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Uadilifu wake mkubwa wa kuondosha maovu yote ya kikoloni yaliyokuwa yanafanyika nchini humu kwa makusudi na bila ya woga wowote. Aidha, wanapaswa kumuombea dua la kheri Marehemu Mzee Karume, lakini kwa ukosefu wa fadhila na kwa unafiki walionao ndani ya nafsi zao, walizidisha fitna pamoja na kupandikiza mbegu za chuki, zenye chembe chembe za dharau na kupambwa na joho la ufedhuli, kejeli na kebehi dhidi ya Mwana Mapinduzi huyo. Kama hiyo haitoshi, bila ya halali na kwa chuki zenu wapinga maendeleo wa Taifa hili walidiriki kumuua Mzee wetu huyo (Karume). Lakini kifo cha Mzee Karume kama Masheikh wanafiki wagekuwa wanafahamu, wanapaswa kutafakari kwa upeo zaidi majina ya viongozi waliofuatia baada ya kifo cha Mzee Karume, kwani mdorongo wa majina ya viongozi hao yanayotoa sura halisi ya kiungwana. Pamoja na ukweli kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoandaliwa na kuongozwa na Mzee Karume, lakini kwa kweli Mapinduzi hao yalipangwa na Mwenyezi Mungu (Subuhanahu Wataala).

Wadhalimu baada ya kumuua Mzee Abeid Amani Karume walidhani wamefanikiwa kuangamiza dhamira ya Mapinduzi, kumbe Mwenyezi Mungu amewapa mtihani wapinga maendeleo hao ili wazingatie na kutafakari kwa nini Mola baada kuuawa Mzee Karume, kamleta Mzee Aboud Jumbe Mwinyi ?. Kwa ufupi , tafsiri yake ni kwamba neno “Aboud” ni mtiifu au kufuata amri. Neno hili amelitumia Mola kwenye Aya Wamakhalaka–ljini wal-insi ila liabudullah – maana yake ni kwamba “sikuwaumba watu na majini ila wanitii. Kwa maana hiyo, Aboud Jumbe ni mtiifu wa Mjumbe yaani wa yale yaliyoachwa na Mjumbe wa Amani. Mafisadi walikwisha jipenyeza ndani ya Serikali ya Mapinduzi, wakala njama za makusudi za kutaka kumtoa Mzee Aboud Jumbe, kwenye madaraka ya Urais wa Zanzibar, ili mafisahdi hao wapate kutwaa madaraka hayo kiurahisi. Mwenyezi Mungu kwa hekma zake, akatupa somo Wazanzibari sote na hatimaye akatuletea kijana mwengine mpya kabisa na mwenye uchungu na Taifa hili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, ili kuchukua nafasi iliyowachwa na Mzee Jumbe.

Kama kawaida, neno Ali maana yake ni muadilifu. Hassan (mwema). Hapa Mola, anatukumbusha uadilifu pamoja na wema aliotufanyia huko nyuma (1964), nasi tukaitikia amri yake na tukawa tayari kwenda “Bomani” na hatimaye kupindua Serikali ya kikoloni hali yakuwa hatuna silaha ya kuaminika. Tumeingia Bomani humo tukiwa na mapanga, mawe na mishale, huku tukijua Bomani kuna bunduki, mizinga na silaha nyengine nzito zaidi na hivyo kuifanya Zanzibar kuweka historia ya aina yake duniani kwa kufaulu kuung’oa utawala wa kisultani kutokana na maandalizi duni nay a muda mfupi mno.

Kuja kwa Rais Ali Hassan, ilikuwa ni ukumbusho na kututahadharisha Wazanzibari kwamba maadui bado wamo ndani ya Serikali na kila uchao wanafanya njama za hujuma dhidi ya Serikali. Kwa upendo wa Mola juu ya waja wake wa Visiwa vya Unguja na Pemba, ametujaalia maajabu makubwa. Utawala wa Mzee Ali Hassaan, ulichukua muda mdogo. Hii ilithibati tosha kuonesha kwamba alikuja kutoa hadhari juu ya maadui hao wa Mapinduzi ya Zanzibar. Ithibati ya usema huu, unatokana na vitimbwi alivyokabiliana navyo aliyekuja kushika Wadhifa huo Mzee Idrissa Abdul- Wakil, baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi, kuachia madaraka.
Mzee Idrisha Abdulwakil nafikiri bila ya shaka wale wataalum kwa lugha ya Kiarabu pamoja na Masheikh na Masheikh wanafanya nini maana Abdul-Wakil, Abdul-Wakil maana yake ni Mjumbe wa kudhukuru kwa maana hiyo Mzee Idrisa Abdul-Wakil ndie kiongozi aliekuja kutoa hokum nani mbaya na nani mwema ndani ya Serikali ya Mapinduzi. Kila mnafiki aliyejitokeza kutokana na hali hiyo, Mzee Idrissa Abdulwakil, alikuwa wakati wote anatimiza kazi yake kwa kutoa hokum dhidi ya wanafiki wote waliojitokeza katika Serikali yake. Hali hiyo iliendelea hadi kufikia muda fulani alipolazimika kulivunja Baraza la Mawaziri na kuwatoa wanafiki wote waliokuwamo ndani ya Baraza hilo. Hakika, Mzee Abdulwakil, ni Kiongozi wa Kwanza kabisa katika Jamhuri ya Tanzania, kuvunja Baraza la Mawaziri. Ukweli usiofichika wale wote aliowafukuzwa kutoka Baraza hilo, ndio hao sasa wamekuwa wapinzani wakubwa wa Serikali (SMZ) pamoaja na Taifa la Zanzibar. Mbaya zaidi viongozi hao wakishirikiana na Masheikh (vilemba) ndio walio mstari wa mbele kupinga na kudiriki kutoa kauli hadharani na bila ya woga kwamba Mapinduzi ya Januari 12, 1964, sio halali wanafiki.


Baada ya kuondoka mzee Abdulwakil, nafasi yake ilichukuliwa na Dk. Salmin Amour (Komandoo). Maana halisi ya neno “Salmin” ni salama mara mbili na “Amour” yaani Amrisha. Itakumbukwa kuwa Rais Salmin Amour, ndie aliyekubali kuanzisha mfumo wa vyama vingi, mfumo ambao maadui waliutaka na kuukaribisha kwa hamu kubwa kwani waliona kuwa wataweza kuutumia mfumo huo kama njia yao yamkato ya kutekeleza azma yao ya kurejea katika utawala wa Kibaraka. Siku ya mwisho ya Kampeni mwaka 1995, kiongozi mmoja wa kundi hilo, alitamka kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Demokrasia (sasa Kibanda Maiti), “eti utawala wa mtu mweusi mwisho leo”. Lakushangaza ni kwamba aliyetangaza kauli hiyo, ni mtu mweusi kama au kuliko makaa (mkaa).

lakini baada ya MOLA kuzima njama zao, walifunga safari kwenda huku na huko duniani, eti kuutaka Ulimwengu uzuie misaada ya kibinadamu kwa Serikali (SMZ), ili jamii ya Waza Zanzibari, iweze kuangamia kwa shida mbali mbali ikiwemo njaa. Kwa uwezo wa Mola (Subhanahu wataala), Mhe. Dk. Salmin (Komandoo), alipambana na njama zote hizo na hatimayejahazi ( Taifa) alilivusha salama. Dk. Salmin alifanya hivyo kwa nguvu zake zote, kwani pamoja na ukweli kwamba hiyo ndio kazi yake lakini kubwa zaidi alifanya hivyo ili kulinda Mapinduzi ya Zanzibar kwa maslahi ya Taifa na watu wake. Wakati huo, mara nyingi, Rais Salmin, alikuwa akiwaliwaza wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa kauli nzuri “tulieni, tulieni, Mola ataleta kheri yake dhidi yetu”. Alikuwa akiwapoza Wazanzibari wakati kauli za mafisadi hao pale alipoona kauli zao zinaashiria shari.

Muda wa Dk. Salmin Amour, ulipomalizika, Wadhifa huo umekamatwa na Rais Aman Abeid. Bila ya shaka tafsiri ya majina haya Masheikh wanayafahamu. “Amani” ni Utulivu na “Abeid” (Mjumbe). Hapa tunakumbushwa kuwa Amani na Utulivu wa nchi hii aliyotuletea Hayati Abeid Amani, kwa uwezo wa Allah, hatuna budi kuulinda kwa nguvu zetu zote. Aidha, tukichunguza kwa makini tutagundua kuwa kazi nzuri aliyoiacha Mzee Abeid, sasa inatekelezwa na Rais Amani Abeid Amani Karume. Lakini si hayo tu, bali tunakumbushwa wema tuliofanyiwa Wazanzibari na Mola wetu kupitia kwa Mzee Abeid Amani Karume. Tunafahamishwa kuwa hao Masheikh vilemba hawafahamu kuwa Wa-Afrika wa Zanzibar waliteswa, kunyaanyaswa na kudharauliwa? Hatupawi kugeuka kama walivyogeuka Mayahudi, kukejili neema walizoteremshiwa na MOLA WETU MTUKUFU AZZA WA JALAH. Tukifanya hivyo, nasi tutaangamizwa kama walivyofanywa Mayahudi.

Jamii ya Wazanzibari na hasa wananchi wapenda amani wote, inajua kwamba wapinga maendeleo hao wameenea kila pembe za Visiwa vya Zanzibar, ili kueneza unafiki wao. Baada ya kuona hawajafanikiwa, hivi sasa wameanza kuleta fitina ya kutugawa kwa kutumia hoja ya Muungano eti si halali na kwamba haukutiwa saini yoyote baina ya Hayati J. K. Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume. Jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, wanajiuliza nini faida watakayoipata iwapo Muungano huo ukivunjika ?. Aidha, watafanikiwa kuiondoa Serikali ya Mapinduzi ya Unguju ?. Hakika huko ni kujidanganya.

Tunawaambia kuwa Muungano wa Tanzania haukuanza mwaka 1964 kama wanavyofahamu. Muungano wa Tanzania umeanza kabla ya kuingia Mjerumani Mrima na Zanzibar, ilikua ni nchi moja. Hivi hawafahamu kwamba Mjerumani ndiye aliyewatenganisha wa Mrima na wa Zanzibar ?. Waangalie watu wa Mrima na wa Zanzibar, kisilka, kimila na kiutamuduni – hakika zinafanana. Watu wake wanauhusiano wa damu. Mfano mzuri - watu wa Bumbwini na wale wa Kipumbwa huko Tanga walivyokuwa na udugu wa damu. Aidha, watu wa Kizimkazi na watu wa Mafia, Dole na Waruguru, n.k. Hivi hawajui watu wa Makunduchi walikuwa wakicheza Benbati, ngoma yenye asili ya Wanyamwezi ?. Ngoma ya Msondo huchezwa na kinamama wa Kilwa na hata wale wa Tanga, Mtwara ?.

Pamoja na hayo, lakini kuna jambo moja ambalo linaagusa Wazanzibari na Watanzania wengi nalo sio jengine bali inasemekana kumejitokeza kundi jengine la watu (Masheikh) linalojiandaa kuhoji kuhusu Pemba na Zanzibar, eti ilikuwaje ikawa nchi moja ?. Kikundi hiki ni sawa na kile kinahoji Uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Lengo lao ni kutaka kuzima NURU YA MWENYEZI MUNGU KWA VINYWA VYAO. Tunasema hawatafanikiwa, kwani Mwenyezi Mungu anawafahamu vyema wanafiki. Namalizia usemi wangu kwa kuwafahamisha hawa Masheikh vilemba kuwa pamoja na uadui walionao dhidi ya Mapinduzi ya Zanzibar, wajuwe Mapinduzi hayo yametayarishwa na kusimamiwa na Mwenyezi Mungu. Ni yeye ndie anayeyalinda na kuyadumisha milele. Kuhusu Muungano wa Tanzania nao pia umeletwa kwa uwezo wake na kwamba kwa baraka zake atausimamia na kuhakikisha kuwa hautavunjika kwa njama za mafisadi hao. Kwa hali hiyo tunapaswa kuamini kuwa hiyo ni neema iliyoletwa na Mola juu yetu na hivyo yeyote mwenye kupinga neema ya Mwenyezi Mungu ni sawa na Kafiri.
“MUNGU IBARIKI TANZANIA”
“MUNGU IBARIKI ZANZIBAR”

MWINYIHAJALI KONDO/ALI NDOTA - ZANZIBAR.

No comments: