Monday, July 9, 2007

Ndugu Mhariri

Naomba nafasi ili niweze kutoa maoni yangu juu ya bei ya mafuta iliyopo hapa nchini.

Ni muda mrefu sasa tokea Bodi ya Mapato nchini kupitia Afisa wake wa kodi kututangazia Wazanzibari kuwa Serikali imejitoa katika kudhibiti bei za mafuta nchini ili wafanyabiashara wa bidhaa hiyo wapange bei kwa mujibu wa gharama halisi za biashara hiyo.

Kutokana na ufahamu wangu mdogo wa biashara nilitegemea kuwa bei ya mafuta nchini hivi sasa ingepungua kama ilivyo nchi nyingi duniani kutokana nakuongezeka uzalishaji hasa nchi zenye kuzalisha kwa wingi mafuta (OPEC). Vile vile, kwa upande wa shilingi ya Tanzania nayo imeimarika kidogo siku hizi thamani yake kuliko kipindi ambacho bei ya mafuta ilipanda hadi kufikia bei Tshs. 1350, kwa Petroli na 1320 kwa Disel. Kipindi hicho dola moja ya Kimarekani ilikuwa niTshs. 1320 kuinunua. Hivi sasa dola moja ya Kimarekani ni Tshs. 1275 kuinunua. Wakati huo huo, Pipa moja la mafuta hapo kabla katika Soko la Kimataifa likiuzwa dola 79 na hivi sasa ni dola 62.

Kwa hiyo,kutokana na mwenendo huo wa bei, kimataifa ilitakiwa bei ya mafuta nchini nayo ipungue hasa kutokana na Serikali kujitoa katika kuhodhi bei ya mafuta nchini na kwa uchache bei iwe kama ilivyo Tanzania Bara ambapo bei hivi sasa kwa lita moja ya Petroli haizidi 1270 hata kwa Mikoa iliyoko mbali na Bandari ya Dar es salaam.

Mwisho ningeiomba Wizara au Idara inayoshughulikia mwenendo mzima wa bei za bidhaa na huduma nchini kufuatilia kwa karibu zaidi bei zinazopangwa na wafanya biashara ambao hawajali maisha ya wananchi wa kawaida bali wanajali faida yao ili mpango wa kupunguza umasikini ufanikiwe nchini kwani kupanda kwa bei holela kwa bidhaa muhimu au kutopungua bei zake hata kama masoko mengine yamepunguza bei zake ni kutomtendea haki raia wa kawaida anaebebeshwa mzigo huo kwa njia isiyo ya moja kwa moja na maana halisi ya kuwepo soko huria itakuwa haina maana. Ni tegemeo langu kwamba Serikali nayo itaingilia kati suala hili pale inapoona kuna wakorofi wachache wanaoweka tamaa mbele kibiashara kuliko urahisia wake.


‘MWANANCHI MPENDA MAENDELEO’


………….
ALI SAID MUSSA
MAGOMENI
ZANZIBAR

No comments: