Monday, July 9, 2007

MAAMBUKIZI YA UKIMWI WA KISIASA

MAAMBUKIZI YA UKIMWI WA KISIASA

Ndugu Mhariri,

NAOMBA nami nikiwa mmoja kati ya wanajamii wa nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nishiriki katika kutoa maoni yangu kuhusiana na tukio la aina yake lilotokea katika medani za kisiasa za Nchi yetu hivi karibuni ambapo Vyama vya Siasa vya kambi ya Upinzani vimesaini Mkataba wa Makubaliano (Memorundum of Understanding) ya kushirikiana katika kupambana dhidi ya Chama Tawala cha CCM.

Vyama vinne vya CUF, CHADEMA, TLP na NCCR – MAGEUZI vikiongozwa na Wenyeviti wao vilikutana katika Ofisi za Makao Mkuu ya Chama cha CUF na kukatibiana kwamba kuanzia sasa vitashirikiana bega kwa began a ikiwezekana zaidi ya hapo katika kuendesha shughuli zao za kisiasa katika kupambana na CCM na Serikali zake na kwamba katika Uchaguzi Mkuu ujao – wa mwaka 2010 vitasimamisha Mgombea mmoja wa Urais na kutozozana katika Majimbo ya Ubunge na Uwakilishi na hatimaye Udiwani na Uenyekiti wa Mitaa na Vitongoji. Vyombo vya Habari vilivyoripoti taarifa hizi waliyapa makubaliano haya majina tofauti wengine walikiita Ndoa, Ushirika na kadhalika.

Mimi kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana viongozi hawa na Vyama vyao kwa kuthubutu kutoka hadharani na kutwambia kwamba wao sasa ni wamoja ingawa Vyama ni tofauti. Lakini niwapongeze zaidi kwa nia waliyokuwa nayo kwamba safai haitoishia hapo, bali ni kuungana kabisa na kuwa Chama kimoja na kupunguza Utitiri wa Vyama katika Kambi ya Upinzani. Sasa tunasubiri kutekelezwa kwa nia yao hiyo njema.

Sasa naomba niweke bayana wasi wasi wangu niliyonao katika ndoa hii. Wanaharakati wa masuala ya jamii siku za hivi kaaribuni wamekuwa mstari wa mbele kabisa kusisitiza umuhimu wa kupima virusi vya UKIMWI kabla ya wanandoa wataarajiwa kufikia uamuzi wa kufunga ndoa zao. Binafsi yangu mimi naungana na wanaharakati hawa sio kwa jengine lolote bali kupunguza kasi ya maambukizi hivi vya Ukimwi (VVU) na hatimaye ndipo tutakapo tokomeza maaradhi hayo dhalili ya Ukimwi.

Sasa najiuliza jee ndoa hii ya wanandoa hawa wanne imepitia utaratibu huu tunaoelekezwa na wanaharakati hawa au ni ndoa ya Mkeka isiyoweza kusubiri achilia mbali kupimwa Ukimwi hata utaratibu mwanana wa ‘posa’ na ulipaji wa ‘mahari’.

Nimejiuliza suala hili kwa sababu Chama cha Siasa ni Chama cha Wanachama na sio cha Viongozi. Hivyo wenye Chama yaani Wanachama wanafahamu kinagaubaga kuhusiana na ndoa hii. Na kama wanafahamu basi hakuna hata mwanandugu mmoja aliyethubutu kutoa tahadhari ya kupima ‘VVU’ wa kisiasa kwanza kabla ya ndoa.

Nina mashaka hayo kwasababu miongoni mwa waliofungishwa ndoa hii mbona wanazo dalili za Virusi vya Ukimwi wa Kisiasa. Narudia kusema mashaka yangu na sio dhambi mwanadamu kuwa na mashaka kwani yananisaidia kuwa mwangalifu. Ukimwi wa kisiasa hauna dawa wala kinga kama Ukimwi ule mwengine. Sasa tutafanyaje wanandoa hawa watakapoambukizana. Si ndio utakuwa mwanzo wa vifo vyao na mwisho wa maisha yao.

Nia yangu ni kuwasaidia na sio kuwavunjia. Kwa maana mimi sina wivu na kati ya yeyote ya wanandoa hawa. Lakini Ukimwi unaua. TAHADHARI kwa wale ambao hawajaoa au kuolewa na hawa.



USHIRIKA MPAKA PEMBA

Tumepokea taarifa ya kuundwa kwa Ushirika wa Vyama vya siasa uliohusishwa Vyama vine kati ya vingi vilivyo katika kambi ya upinzani. Vyama hivi ni CUF, CHADEMA, TLP na NCCR – MAGEUZI.

Siasa za Vyama vingi zilizoanza rasmi hapa Tanzania mwaka 1992 zinatupa picha ya kuwa takriban kila Chama kina eneo lililolidhibiti ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nikitolea mifano, CCM imedhibiti eneo karibu lote la Tanzania, isipokuwa kule Pemba. Ambapo TLP ina wanachama wengi zaidi Kilimanjaro ya Uchagani, UDP Shinyanga hususan Wilaya ya Bariadi.

Katika Ushirika huu ulioundwa pale Buguruni Dar es Salaam tarehe 10/05/2007 Chama cha CUF kimejidhihirisha kuwa katika ndoa hii ndio Chama pekee chenye eneo la kujidai, ambapo tokea uchaguzi wa kwanza wa Vyama vingi mwaka 1995 wamelidhibiti hadi sasa. Eneo hili ni eneo lote la Kisiwa cha Pemba kule Zanzibar.

Tabaan mwaka 2003 ulipofanyika uchaguzi mdogo kwa baadhi ya Majimbo ya kule Pemba na baadhi ya Wagombea wa Chama cha CUFkuenguliwa katika orodha ya wagombea wanachama na wafuasi wao waliamua kupigia kura “maruhani” baada ya wagombea, wa vyama vyengine vilivyogombea. Matokeo ya uchaguzi ule yalidhihirisha umwamba na undava wa CUF ndani ya Pemba. Walioshinda katika Majimbo ambayo hayakuwa na wagombea wa CUF walipata kati ya kura 300 na 1000 miongoni mwa takriban kura 4000 hadi 5000 zilizopigwa. Waliogombea pamoja na CCM walikuwepo waliowakilisha Vyama vya Upinzani na zaidi walikuwa wagombea wa NCCR-MAGEUZI na TLP, ambao sasa ni miongoni mwa wanandoa/wanaushirika huu ulioundwa.

Wana haarakati wa masuala ya kisiasa hapa ndipo wanapouliza masuala yao kuhusiana na Ushirika huu. Je kweli kwa makubaliano haya, Chama cha CUF watakuwa tayari kuachia sehemu ya Majimbo yake ya Pemba kwa TLP, CHADEMA au NCCR – MAGEUZI, ili kuimarisha upinzani kule Zanzibar na kujenga nguvu za pamoja za kupambana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na CCM Zanzibar. Kama hii itawezekana na tunaomba Mwenyezi Mungu iwezekane litafungua ukurasa mpya katika harakati za kisiasa nchini na litadhihirisha upevu wa kisiasa kwa viongozi wa Vyama hivi. Lakini endapohili halitawezekana na hatuaombi iwe hivyo, litathibitisha ule usemi wa Kiswahili usemao “CHAKO CHETU, LAKINI CHANGU CHANGU”. Hali hii siyo tu italeta ufa katika ushirika huu bali utakuwa mpasuko na mwisho wa ushirika.

Kuwa kuwa ushirika huu umeshatiwa sahihi na kubarikiwa na Vyama hivi, tunafikiri pahala pazuri pa kuanzia kudhihirisha nia njema ya viongozi hawa katika kushirikiana wasisubiri mwaka 2010 au kuweka shinikizo la mabadiliko ya Katiba na Tume ya Uchaguzi. Bali Chama cha CUF kupitia kwa Kiongozi wake ndani ya Baraza la Wawakilishi apeleke mapendekezo ya Makada kutoka TLP, CHADEMA na NCCR – MAGEUZI kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ili miongoni mwao wateuliwe kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika nafasi kumi za Rais. Hili likifanyika na ni vyema likafanyika sasa litajenga mshikamano wa dhati ndani ya ushirika huu.

Vinginevyo badi hatubaki na mashaka yale yale ya kwambva “chako chetu, lakini changu changu”.

Wakiweza kufanikisha hili la mashirikiano ya dhati, watatuthibitishia kuwa ushirika huu ni kwa Jamhuri nzima ya Tanzania ikiwemo na Pemba. Lakini ikifanyika vinginevyo itakuwa ushirika bila ya kuhusisha Pemba. Na kwa maana nyingine ushirika mwisho Nungwi.

Tunawatakia kila la kheri. Lakini tuanze sasa tusisubiri mwaka 2010.

No comments: