Monday, July 9, 2007

KILEMBA CHA UKOKA

TUNAWAAOMBIA CUF WAACHE KUMVISHA KILEMBA CHA UKOKA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO MHE.JAKAYA MRISHO KIKWETE
Ni kweli dunia ina vituko. CUF baada ya kumkejeli Rais Kikwete wakati wa Uchaguzi Mkuu, leo wanamwendea kumuomba awasaidie ili aandae mazingira yatakayowezesha kuundwa Serikali ya mseto Zanzibar. Viongozi wa CUF waliyoshindwa na CCM, wapewe nyadhifa za juu Serikalini kwa kile wanachokidai kuondoa mpasuko wa Kisiasa. CUF hawamjui Rais Kikwete na wahenga wamesema “Jambo usilolijua ni usiku wa kiza”. Si dhani kwamba itakuwa jambo la rahisi kwa Mhe. Rais Kikwete kukubali matakwa yao. Hivi karibuni Wana CCM Zanzibar walifanya maadhimisho kwa ajili ya kusherehekea mwaka mmoja wa ushindi wa CCM uliopatikana katika Uchaguzi Mkuu wa Octoba 30, 2005. Kwenye maadhimisho hayo wamempongeza Rais wao Mhe. Karume. Naye amepokea pongezi hizo kwa furaha na bashasha kubwa. “Tunaendelea kwenye shughuli muhimu za kujiletea maendeleo yetu kwa faida ya wote bila kujali Itikadi za kisiasa. Mabarabara, nyumba, Mashule, Hospitali na tunaendelea kuimarisha Uchumi wetu kwa kasi isiyo na kifani kupitia Sekta mbali mbali”. Alisema Rais Karume kwenye mkutano huo wa kujipongeza.

La kushangaza ni kwamba Viongozi wa CUF baada ya kuona ukweli kwenye maendeleo yetu wameamua kwenda kumuona Rais wetu mpendwa Mhe. Kikwete, eti awasaidie kubatilisha Ushindi wa CCM kwa kile wanachokiita “Uchaguzi sio huru na haki” na kwamba CCM imefanya udanganyifu – imepora ushindi wa CUF. Jee hilo linakubalika au janja yao?

Tunawaambia CUF watambue kuwa hilo haliwezekani. Wasijigambe kutaka kumvisha kilemba cha ukoka Rais wetu. Hivi juzi kwao alikuwa ni kiongozi asiye na uwezo, leo awe na uwezo wa kukiuka Katiba ya CCM na Serikali zake kwa kubadili Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iwe ya Mseto wa CCM na CUF? Hilo ni kujidanganya kupita kiasi.

Sisi tunafahamu fika ujanja wa CUF kuwa ni urithi wa asili wa Chama Cha Hizbu na bwana wao Sultani. Hizbu yaani ZNP ilikuwa daima dawamu haikubali ushindi wa ASP. Katika chaguzi zote zilizo fanyika takriban mara nne hapa Zanzibar tangu 1957 – 1963, kwa mizengwe na ukaidi wa Hizbu, ASP ilishinda karibu katika chaguzi zote hizo, lakini ushindi haikupewa.

Lakini hata baada ya nchi yetu kurejea katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwanzo chini ya Demokrasia hii mwaka 1995 na 2000 na wa mwaka 2005, CUF haijakubali kushindwa pamoja na kwamba mara zote hizo wameshindwa kweli kweli. Kiongozi wa CUF Seif Sharifu Hamadi hajapata kukubali kushindwa mahala popote alipogombea. Kila Uchaguzi unapofanyika akishindwa anadai urejewe tena eti alifanyiwa mizengwe.

Majuzi Wabunge wa CUF walitaka kueleza maelezo hayo hayo ndani ya Bunge. Sasa kwa kuwa wanaona Chama chao (CUF) kila uchao kinadidimia, hakina pa kushika wanabuni mbinu za kuwatuliza wafuasi wao wasisambaratike.

Baada ya kushindwa na CCM katika Uchaguzi uliopita, sasa wameamua kuwmendea Mhe. Rais Kikwete kumuomba amshawishi Mhe. Amani Abeid Karume aunde Serikali ya mseto kwa Zanzibar. Seif ameashau kwamba Rais Kikwete alitaraji kuungwa mkono na wafuasi wa CUF Pemba pamoja na kuwa na wafuasi wake wengi Unguja na Tanzania Bara. Hilo hakuliona, wakati ule alimsema kuwa ni Rais asiye na uwezo, akidai kuwa yeye na Lipumba ndio wanaofaa zaidi.

Jee, leo Seif kumpigia magoti Rais Kikwete huoni aibu? Ndipo kwa sisi Wana CCM tunateta kua anamvisha kilemba cha ukoka Rais wetu. Hilo haliwezekani wala halivumiliki kwa upande wa Wana CCM.

Katika tamko walilotoa viongozi wa CUF wamesema kuwa wanamuunga mkono Rais Kikwete kwa matamshi yake kuwa atashughulikia mpasuko wa Kisiasa Zanzibar kwa dhana kwamba ataifanya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iwe ya mseto na hivyo CUF kumuona Rais Kikwete kuwa ni Mkombozi wao.

Sisi Wana CCM, Wakereketwa na Wapenda amani tuliopo Zanzibar tunaona kama CUF wanacheza mchezo wa kitoto kwa kudanganyana. Maana sasa Uchaguzi umekwisha, Serikali zimeshaundwa na zinafanya wajibu uliokusudiwa. Kilichobaki sasa wana CCM na Wana CUF ni kushirikiana vizuri katika ujenzi wa Taifa letu sio kusubiri mseto. Huo ndio uzalendo unaohitajika sasa. Pale wanapoona pana makosa wasaidie kukosoa kwa maslahi ya Taifa badala ya kusubiri iundwe Serikali ya mseto. Tunawaambia wana CUF kwamba Uchaguzi uliopita umekwishapita hivyo wajiandae kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, maana Katiba ya Tanzania inatamka kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika kila baada ya miaka 5. Tunasema tena kwamba haifai wana CUF msijidai kumvisha Rais wetu kilemba cha ukoka.

“MAPINDUZI DAIMA”

“MSETO ZII”

No comments: