Monday, July 9, 2007

USHINDI WA 2005

Ushindi 2005 Zanzibar hautopatikana kwa jazba

Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea kwa kasi, Chama Cha Wananchi (CUF) kimeshajitangazia kushinda kiti cha Urais Zanzibar hata kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika. Mwandishi Wetu ALLY MWINYIKAI anabainisha iwapo ni vyema kufanya hivyo au la, endelea…

Nadharia ya chama kushinda ina maeneo mapana na kwa kweli ni safari ndefu sana. Mbali ya kuhitajika kuwepo maandalizi ya kutosha lakini kunatakiwa kufanywa tathmini ya hali ya juu katika kila hatua inayochukuliwa katika kuelekea kwenye uchaguzi wenyewe.

Moja ya hatua ya kwanza na muhimu kuliko zote ni uandikishaji. Uandikishaji wapiga kura ni muhimu kuliko jambo lolote jengine. Umuhimu wa jambo hilo kwa Zanzibar ulianza kuonekana waziwazi tangu uchaguzi wa mwanzo wa vyama vingi nchini uliofanyika mwaka 1995.

Umuhimu huo ulijitokeza baada ya kubainika kasoro kubwa zilizofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) upande wa Zanzibar. CCM kilijiamini sana kwa kuwa na wafuasi wengi na hata kubweteka kwa kutotilia uzito unaostahili suala la kuhimiza wafuasi wake kujiandikisha.

Chama hicho kilionekana kutosheka na wingi wa wafuasi iliokuwa nao ambao wakijazana katika mikutano ya hadhara hadi kufikia kutunga nyimbo maalumu iliyokuwa ikisema, “CCM watu kibao.”

Hiyo ni kasoro ambao haijapata kuzungumzwa hadharani kwa karibu miaka 10 sasa, lakini ilikiathiri kwa kiasi fulani chama hicho kwa kuruhusu ushindani wa kisiasa kuonekana mkubwa Zanzibar kuliko sehemu nyingine za Tanzania.

Watafiti wa mambo ya kisiasa Zanzibar walichunguza kutaka kufahamu kwa undani mambo yaliyosababisha chama hicho kupata ushindi mwembamba katika uchaguzi huo licha ya kuwa na wafuasi wengi.

Ugunduzi wa utafiti wao ulibaini mambo mengi ya ghilba na hadaa yalizofanyika ambayo nayo hajatangazwa mahala popote. Miongoni mwa mambo hayo ni wafuasi wa CUF kisiwani Pemba kujifaragua watakavyo ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu kuruhusiwa kupiga kura zaidi ya mara tatu.

Sehemu moja ya ugunduzi huo ni kuonekana kwamba kulikuwa na kundi kubwa la vijana la wafuasi wa CCM lililohamasika sana wakati wa kampeni za uchaguzi huo lakini lilikuwa halikujiandikisha.

Ilikuwa ni dosari ambayo ilirekebishwa katika uchaguzi uliofuata wa 2000. Kurekebishwa kwa kasoro hiyo kulitoa nafasi ya baadhi ya wachambuzi waliokuwa hawakuvutwa na hisia za kisiasa za upande mmoja kutabiri mapema nani angeibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Hapana shaka, matayarisho ya uandikishaji wapiga kura katika uchaguzi wa 2000 yalidhihirisha wazi kwamba CCM ingeshinda na hata wapinzani walioshiriki uchaguzi huo waliuchukulia uchaguzi huo kwa tahadhari kubwa. Tahadhari hiyo ndio mara ilipopatikana fursa ya kugomea, CUF waliitumia ipasavyo.

Ni katika uchaguzi huo, Chama cha Wananchi (CUF) kilisusia kushiriki katika uchaguzi wa majimbo 16 ya Mkoa wa Mjini/Magharibi, hapana shaka kwa kuelewa kwamba hakukuwa na mwanya wa chama hicho kushinda zaidi ya kuendeleza wimbo wake wa kuibiwa kura.

Hakukuwa na njia nyingine ya CUF kufanya katika uchaguzi huo hasa kwa kuzingatia kwamba chama hicho kilikuwa kimeshawaahidi wafuasi wake kushinda katika uchaguzi huo kutokana na tamaa iliyokuwepo kwa kuangalia ushindi mwembamba wa uchaguzi wa 1995.

Kauli za chama kimoja kutamka kushinda na baadaye kugeuza kibao cha kuibiwa kura inaonekana kuanza kuota mizizi hivi sasa kutokana na kusikika kwa matamshi ya kushinda katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu. Kauli hizo zimeshatolewa na viongozi wa CUF.

Matamshi ya viongozi hao kwa kiasi kikubwa yameanza kuvuta hisia za wafuasi wa chama hicho kwa kuyaamini na hasa wafuasi wasiokuwa na nyenzo za kufanyia uchambuzi wa kina juu ya masuala ya siasa na mwenendo mzima wa uchaguzi unavyokuwa.

Kitu kikubwa kinachoangaliwa katika uchaguzi wowote ni idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura na wanaoshiriki katika zoezi hilo siku ya uchaguzi yenyewe. Wakati viongozi hao wa CUF wanajitangazia ushindi wanaelewa wazi kwamba ni watu 157,343 Pemba na watu ……. wameorodheshwa Unguja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura la Zanzibar.

Wasiwasi huo unakuja kwa kuangalia nguvu za vyama vinavyotegemea kushiriki katika uchaguzi huo na maeneo ambayo vyama hivyo vina ngome zao. Hapana anayepinga kwamba CUF inawafuasi wengi katika kisiwa cha Pemba ikilinganishwa na CCM ambayo ngome yake kubwa iko Unguja.

Hivyo, kinachoonekana katika jitihada za wanasiasa kujitangazia ushindi ni kutaka kuendeleza hisia za kuvuruga mawazo ya baadhi ya wafuasi wa vyama na kuanza kujiwekea kinga mapema ili matokeo yatakapokuwa kinyume na matamshi ya awali kujengwa dhana ya kuibiwa kura.

Historia inaonesha chanzo cha machafuko ya kisiasa ya hivi karibuni kilitokana na CUF kujitangazia ushindi mwaka 1995 kupitia idhaa moja ya Televisheni hapa nchini kwa kutoa matokeo ya kubuni. Kutangazwa matokeo halisi suala la kuibiwa kura ndipo lilipoibuka na vurugu kuenea.

Muafaka uliofikiwa kati ya vyama vya CCM na CUF unatanabahisha kuepukwa jazba zinazochochea chuki na uhasama pamoja na kusisitiza kusahauliwa ya nyuma. Kujitangaza kushinda kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wenyewe hakuelekei kujenga mazingira hayo.

Kwa mwelekeo huo, lengo la kujenga mazingira mapya ya kuaminiana katika uendeshaji wa siasa nchini linatoweka. Kauli za kutokubali matokeo ya kushindwa katika uchaguzi ujao zinajitokeza. Aidha, zinaonekana hisia za uchochezi wa uvurugaji wa amani na zinazotishia kutothaminiwa kwa makubaliano yaliyofikiwa kwenye muafaka huo.

Kuna haja ya kujenga mazingira mazuri ya kudumisha ustaarabu wa kisiasa wa kupingana bila ya kupigana na kushindana bila ya kuzozana ingefaa katika kipindi hiki cha uandikishaji. Viongozi wa vyama wawahamasishe wafuasi wao wenye sifa za kujiandikisha kujitokeza kutumia haki yao hiyo bila ya kuwapandisha jazba za kurejea miaka ya nyuma.

Tamko la hivi karibuni lililotolewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba chama chake kitafanya ‘mapinduzi yenye muundo wa Ukraine’ haliashirii kuendeleza msisitizo huo wa Muafaka zaidi ya kuwatia hofu wananchi na dunia kwa jumla.

Ubaya wa tamko hili ni kwamba limefanywa kwa kujificha. Kama ilivyo kawaida ya kiongozi huyo ya kutangaza mambo ya hatari anapokuwa nje ya nchi na kujifanya mwema awapo nchini, amelitoa tamko hilo alipokuwa akizindua kampeni ya chama chake huko Nairobi nchini Kenya.

Ni jambo la kushangaza kusikia kiongozi wa Tanzania anazindua kampeni zake za uchaguzi Kenya mahala ambako hakuna wapiga kura. Inaonekana kwamba kiongozi huyo alifanya hivyo kwa kutafuta kuungwa mkono lakini matokeo yake imezusha hofu, woga na wasiwasi.

Wasiwasi umewaingia watu wengi kiasi cha Ofisi ya Ubalozi wa Marekani nchini kuchukua hatua ya kutoa tahadhari kwa raia wa Marekani ili wasitembelee Zanzibar katika kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi huo kwa kuhofia kutokea ghasia na vurugu.

Chanzo cha tahadhari hiyo ni kauli ya kiongozi huyo anayegombea urais wa Zanzibar ambaye hapana wasiwasi wowote ameshabaini kushindwa kwake lakini bado anaonekana kutokubali matokeo yatakavyokuwa kwani ameshatamka kuyakataa hata kama atashinda.

Mara kadhaa, Katibu Mkuu wa CUF amekuwa akitoa matamshi yake ya vitisho kwamba nguvu ya umma itatumika kwa kuandaa maandamano kupinga kile anachodai uonevu unaofanywa na CCM na serikali zake kuhusiana na masuala ya uchaguzi.

Lakini kabla ya hata mzozo huo kuhusu idadi ya wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura haujatokea, tayari kulikuwepo na chokochoko kutoka chama hicho kuhusiana na uchaguzi mkuu huo.

Katika kipindi cha uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari hilo kulijitokeza matukio kadhaa ya kusikitisha huko Pemba ambapo miongoni mwa matukio hayo ni kumwagika kwa damu ambapo chimbuko lake lilitokana na baadhi ya wafuasi wa CUF kujaribu kujipima nguvu na vyombo vya dola.

Baadhi ya viongozi waandamizi wa CUF walikwishatamka wazi kuwa damu itamwagika wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka huu kwa kile wanachodai kuwa ikiwa wataibiwa tena kura kwenye uchaguzi mkuu.

Katika kutoa vitisho hivyo vya umwagaji damu, viongozi hao wa CUF wamekuwa wakikaririwa mara kwa mara wakisema kuwa watahakikisha kuwa mgogoro huo wa Zanzibar unasambaa nchi nzima na wala siyo Zanzibar peke yake.

Mbali ya vitisho hivyo, viongozi kadhaa wa CUF pia wamekuwa wakiendesha propaganda chafu dhidi ya CCM, ambapo wamekuwa wakiituhumu eti CCM ina vikundi vya mauaji vilivyobatizwa jina la ‘Janjaweed’ linalotumika huko Sudan katika kuendesha mauaji huko.

Kwa kuzingatia kauli za viongozi hao wa CUF, hali ya utulivu inaweza ikatiliwa mashaka. Kauli za viongozi hao, kimsingi, haziwezi kupuuzwa, kwani zinaweza kuchochea ghasia na kuitumbukiza Tanzania kwenye mgogoro wa kisiasa, fujo na ghasia.

Hisia hizo za kuibiwa kura zilianzishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho mwalimu Seif Sharif Hamad toka alipokuwa chama cha Mapinduzi. Mwaka 1985 ndani ya mfumo wa chama kimoja alidai kuibiwa kura, Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM ilipomteua Mzee Idris Abdul Wakil kuwa mgombera urais wa Zanzibar na kumwacha Hamad. Kilio hicho cha kuibiwa kura kikitlewa tena katiak uchaguzi wa mwaka 1995 na 2000.

Lakini wakati tukitafakari jambo hilo kuna haja ya kufahamu sababu za kutokea vitisho vya aina hiyo. Sababu hasa ni wapinzani na Maalim Seif kutokubali kushindwa katika uchaguzi wowote wanaoshiriki.

Kauli za aina hii zinaonesha jinsi CUF kinavyojiandaa kutaka kuitia nchi katika misukosuko ya kisiasa na kusitisha kasi ya maendeleo ambapo Serikali itapaswa kujidhatiti vya kutosha kudhibiti hali hiyo.

Aidha, wananchi nao kutokubali kutishika kwa kauli hizo kwa kutowaunga mkono viongozi wenye kutoa kauli za vitisho. Hivyo, wananchi wasipoteze fursa ya kutumia haki yao ya kushiriki katika kuchagua viongozi wanaowapenda.


Mwisho.

No comments: