Wednesday, July 18, 2007

JEMBE NA NYUNDO SIO MSALABA

JEMBE NA NYUNDO SIO MSALABA

WATANZANIA wa rika yangu yaani wale wote wenye umri wa miaka hamsini na kuendelea waliozaliwa kabla na baada ya kuingia Wakoloni katika nchi mbali mbali Barani Afrika ikiwemo Tanzania, walikuwa mashuhuda wa jinsi wakoloni hao walivyolivamia Bara letu hili na kuwatawala wazee wetu ikiwa ni pamoja na kuwakandamiza, kuwanyanyasa na kuwatesa wananchi wake bila sababu ya msingi. Wakoloni hao walikuja kadhaa za Bara la Ulaya ikiwemo Uingereza, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi n.k. walimimika kwa wingi Barani Afrika na kugawana mapande ya ardhi ambayo ni Mali halali ya Waafrika na kuanza kuzikalia nchi hizo pamoja na kuwatawala wananchi wake kwa mabavu. Sina haja ya kuelezea kwa upana zaidi juu ya madhila waliyoyapata mababu na wazazi wetu kwa wakati huo, kwani yanaeleweka kwa kila mtu wa Bara hili.

Kuna sababu nyingi zilizochangia kufanyika kwa uvamizi huo. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba wavamizi hao (Wazungu) walijua kuwa Barani Afrika ndilo bara pekee lenye kumiliki mali ghafi nyingi za aina kwa aina ambazo ni pamba, katani, buni, pareto, korosho, mbata, karafuu, n.k. Kama wangezipata bidhaa hizo zingewasidia kwa kiasi kikubwa sio tu kuimarisha viwanda vyao bali pia zingewaletea mapato makubwa zaidi na hivyo kuweza kujitajirisha na kuwa mataifa makubwa kama yalivyo hivi sasa. Waalifanya hivyo kwa vile Waafrika wenyewe walikuwa bado wapo kizani hadi wakafikia mahali wakaliita bara la watu wakizani (bara jeusi). Haya yote yalikuja kutokana na idadi kubwa ya watu wake walikuwa hawahui kusoma na kuandika.

Wahenga walisema “kila penye mbaya wako na mwema wako yupo”. Pamoja na ukweli kuwa wakoloni walikuwa watu wabaya, lakini pia walikuwepo wengine wazuri. Wakijua kuwa watu wanaowatawala hawana elimu kabisa. Wale wenye mioyo mizuri walijaribu kuanzisha shule (skuli) katika badhi ya nchi barani humu na kuwapatia masomo angalau ya kujua kusoma na kuandika. Hali hiyo iliendelea kidogo kidogo hadi kufikia hapa tulipo na kwamba baadhi ya Waafrika waliweza kupata elimu nzuri kiasi cha kujivunia. Aidha, wakiwa na na hivyo kuweza kuelekeza nguvu zaidi katika mapambano dhidi ya wakoloni hao na kadri siku zilivyosonga mbele ndio mapambano yalizidi kupamba moto hadi kufikia Bara zima kuwa huru.

Mapambano ya kutafuta uhuru kwa kila nchi ya Bara la Afrika yalisimamiwa na baadhi ya wana haraka wa nchi husika. Mathalan, aliyeongoza mapambano ya kutafuta uhuru wa nchi iliyokuwa Tanganyika iliyokuwa chini ya Ukoloni wa Kijerumani ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Visiwa vya Zanzibar, vilivyotawaliwa na Ukoloni wa Kisultan wa Oman, alikuwa Hayati Mzee Abeid Amani Karume. Watu wengine mashuhuri waliosimama kidete kuhakikisha nchi zao zinakuwa huru ni Jomo Kenyatta (Kenya), Kwame Nkurumah (Ghana), Ahmed Ben Bella (Tunisia), Ahmed Sekouture (Guinea), William Tolbert (Liberia), Kenneth Kaunda (Zambia), Nelson Mandela (SA), n.k. Hao ni baadhi tu lakini kuna wengine kadhaa walioongoza mapambano hayo katika nchi zao hadi kufikia ukombozi kamili.

Mwalimu Julius K. Nyerere, chini ya Chama cha TANU, aliongoza mapambano ya kutafuta uhuru wa Tanganyika kwa muda wa miaka saba (7) – yaani 1954 hadi Disemba 09, 1961, ambapo Tanzanyika ilipopata uhuru. Kwa upande Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, chini ya Chama cha Afro Shirazi (ASP), naye kwa muda wa miaka isiyopungua sita (6), aliongoza mapambano dhidi ya ukoloni wa kisultani kuanzia 1957 - Januari 12, 1964, Zanzibar ilipojikomboa katika madhila ya ukoloni na hivyo kuleta faraja kubwa kwa wananchi na hasa wazalendo wa Unguja na Pemba.

Kutokana na busara na hekima za Mzee Karume na Mwalimu Nyerere, kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na Tanganyika, waliweza kuziunganisha nchi hizi mbili hapo Aprili 26, 1964 na kuifanya kuwa nchi moja iliyojulikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na kuungana huko lakini Serikali ziliendelea kubaki mbili ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzanai (SMT), iliyoongozwa na Mwalimu J. K. Nyerere na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), chini ya Uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume. Aidha, baada ya tukio hilo kubwa la kihistoria, Mzee Abeid A. Karume, alikamata Wadhifa wa Makamo wa Rais wa SMT. Lengo kuu la Muungano huo linaeleweka na kila mmoja wetu nalo sio jengine bali ni kuimarisha zaidi masuala ya ulinzi wa ndani na nje ya mipaka yetu.

Tangu kuasisiwa kwa Muungano huo, Watanzania tumeshuhudia mambo mengi ya maendeleo yaliyosimamia kwa ujasiri na umahiri mkubwa wa viongozi wetu hao. Lakini kuwa na jambo moja la msingi la kujiuliza na kila Mtanzania ? Iweje nchi ya Muungano yenye Rais mmoja iwe na Vyama viwili tofauti ?.

Ilichukua muda wa miaka takriban kumi na mitatu (13), ambapo Watanzania waliposhuhudia Viongozi wao wa Vyama vya TANU na ASP – yaani Mwalimu Julius . K. Nyerere na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi (Awamu ya Pili), wakiamua kwa kauli moja na kuviunganisha Vyama hivyo na kuwa Chama Kimoja, Chama chenye nguvu na imara zaidi. Aidha, uunganishaji wa Vyama hivyo kungeweza kujibu suali lililojengeka na kutawala nafsi za Watanzania walio wengi kwamba itawazekanaje nchi yenye Rais mmoja iwe na vyama viwili vyenye itikadi moja ?.

Jibu la suali hili lilipatiwa ufumbuzi Februari 5, 1977, wakati Vyama vya TANU na ASP, vilipoungana na kufanya Chama Kimoja cha Siasa kilichojulikana kwa jina la CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM). Lakini kuzaliwa kwa CCM halikuwa ni tendo la kihistoria tu, bali pia kilikuwa ni kitendo cha kimapinduzi kwa vyama vya TANU na ASP, kukubali kujivunja vyenyewe kwa hiari, heshima na taadhima na kuunda Chama Kipya. Vilifanya hivyo ili kuweza kuendeleza harakati za Ukombozi wa Tanzania. Aidha, kitendo hicho ni uthibitisho tosha wa kukua na kukomaa kifikra, kinadharia, kivitendo na kimuundo kwa TANU na ASP. Kwa mantiki hiyo, wazo la kuunganisha vyama hivyo halikuwa jambo jipya kwa ASP na TANU. Mathalan, ASP ni matokeo ya Muungano baina ya ‘African Association’ na ‘Shirazi Association’.

Hivyo, kuzaliwa kwa CCM ni kitendo dhahiri cha kutekeleza Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965 iliyosema “Kutakuwepo Chama Kimoja cha Siasa katika Tanzania …. Mpaka Vitakapoungana Chama cha TANU na ASP (ambavyo vikiungana vitaunda Chama Kimoja cha Siasa), lakini kwa sasa Chama cha Tanganyika kitakuwa TANU na Zanzibar kitakuwa Chama cha ASP”.

“Mwenye macho haambiwi tazama”. Kila Mtanzania amejionea mwenyewe jinsi CCM ilivyopania kuondoa kero mbali mbali zilizoikumba jamii ya Tanzania na kuleta maendeleo endelevu nchini humu kwa maslahi ya jamii nzima. Miongoni mwa mambo yaliyopatika ni pamoja na kuimarishwa kwa Mmiundombinu ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii, Mawasiliano, Afya, Elimu, n.k. Kama hiyo haitoshi, CCM imeweza kufanikisha azma yake ya kudumisha amani na utulivu wa Taifa letu.

Jambo la kushangaza na kwa kweli linasumbua kwa kiasi kikubwa nafsi za Watanzania walio wengi ni ile kauli ya kupotosha inayotolewa na kusambazwa na baadhi ya Watanzania kwamba “CCM SIO CHAMA CHA WANANCHI WA TANZANIA NA KWAMBA NEMBO YA JEMBE NA NYUNDO ILIYOMO KWENYE BENDERA YAKE NI ALAMA YA MSALABA”. Hakika, kauli hiyo na nyengine kama hizo ni za kupotosha.

No comments: