Wednesday, July 11, 2007

WAPINZANI KUSHINWA KABLA YA UCHAGUZI

Wapinzani wameshindwa hata kabla ya uchaguzi

Wakati tunakaribia katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar imebainika wazi kwamba hofu imewakumba wapinzani na hasa Chama cha Wananchi (CUF) kiasi cha viongozi wao kuashiria kushindwa kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.

Dalili za kushindwa zianza zamani, pengine kabla ya kuanza kamapeni. Hofu hiyo iliibuka mara ya baada ya Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kutangazwa kugembea tena nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi m(CCM).

Kabla ya mchakato wa kumpata mgombea huyo, wapinzani walikuwa wakifanya vibweka vingi huku wakijigamba kuwa wataing’oa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 30, mwaka huu.

Matumaini makubwa waliyokuwa nayo CUF ya kuishinda CCM yalitokana na mawazo yaliyokuwepo kwamba kuna utofahamiana miongoni mwa viongozi wa CCM na hivyo kuweka tama ya fisi ya kutegemea kudongoka mkono wa binadamu.

Kimsingi, mawazo hayo yaliyobeba hisia za propaganda chafu yalikuwa na malengo ya kutaka kuwahadaa wafuasi wa CCM na kuwachanganya viongozi wao kabla ya kuanza mchakato wake wa kumpata nahodha atakayeipeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha urais.

Katika kuiangalia propaganda hiyo, imebainika dhahiri kwamba ilitokana na woga, hofu na waswasi wa kuangushwa vibaya katika kinyang’anyiro hicho,
Baada ya wapinzani kutofanikiwa hila zao za kuingiza mamluki katika uandikishaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura.

Si hivyo tu, lakini CUF katika kujitafutia uhalali wa kuwa chama pekee chenye upinzani wenye nguvu Zanzibar, kilijaribu sana kutaka kuvizuia vyama vingine vya upinzani visiweke wagomea katika nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Mbinu hiyo ilikuwa ni kutaka kuhakikisha kwamba wafuasi wote wa upinzani wanampigia kura mgombea wa CUF katika nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar.

Hilo halikuwezekana kwani vyama vitano vimejitokeza kuweka wagombea wao. Vyama hivyo ni CCM, CUF, Jahazi asilia, UDP na

Kutokana na hali hiyo, inajitokeza wazi kwamba uchaguzi wa mwaka huu, mambo yatakuwa mambo kweli kwani takriban vyama vyote vilivyosimamisha wagombea wao vimeadhimia kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na sio kuibeba CUF ambayo hivi sasa inahitaji kupatiwa msaada wa damu kutoka kwa vyama hivyo.

DALILI ZA KUSHINDWA
Wakati wakujifaragua kwamba mwaka huu lazima CUF ipate ridhaa ya wananchi kuongoza dola, majinato yao yamekoma baada ya hila zao nyingi kushindwa.

Hila za CUF zilianza kukwama tokea wakati wa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulipoanza kisiwani Unguja. Kilichoandaliwa na chama hicho katika uandikishaji huo ni kupandikiza watu wasio na sifa za ukaazi.

Kwa kutumia wafuasi wa chama hicho wanaoishi katika mikoa ya Tanzania Bara, Kenya na nchi za Ghuba, CUF ilijipanga kuandiokisha wapiga kura wengi. Mbinu hiyo iligunduliwa na CCM kwa kutotoa mwanya wa kuandikishwa wasiohusika kwenye daftari hilo la wapiga kura.

Kushindwa kwa mbinu hiyo kuliishia kwa chama hicho kutoa malalamiko yaliyodai kutoandikishwa wafuasi wao wapatao 10,000. Malalamiko hayo yalikuwa ni kuashiria kukubali kushindwa.

Kwa kufahamu kwamba idadi ya walioandikishwa kwenye daftari la wapiga kura haiwezi kukipatia CUF ushindi katika Uchaguzi Mkuu, hila ya kutaka kulichafua daftari hilo zilionekana kushamiri. Kwa kuitumia kampuni ya Waymark kulijitokeza ishara za wazi za kiharamia zilizofanya na kampuni hiyo.

Miongoni mwa uharamia uliofanywa na kampuni hiyo ni kuibwa majina ya wapiga kura 30,000 baada ya kampuni hiyo kuruhusiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuhakiki kwa majaribio majina ya wapiga kura 10,000.

Aidha, mipango ilikuwa inafanywa na kulisafirisha nje ya nchi daftari la wapiga kura kwa kisingizio cha kwenda kulihakiki ili kubaini majina ya wapiga kura wanaofaa na wasiofaa. Kitendo hicho kilikuwa ni cha kutiliwa mashaka makubwa hasa baada ya kubainika wizi uliokwishafanyika wa majina 30,000 ya wapiga kura.

CCM ilitegua mtego huo uliowekwa ambao ulikuwa na mkakati maalumu wa kuharibu daftari hiyo kwa maslahi ya kuwapendelea wapinzani. Kugunduliwa kwa mtego huo pia kulipelekea CUF kulalamika kiasi cha kutishia kugomea kushiriki kwenye uchaguzi wenyewe iwapo hakukufanyika uhakiki. Malalamiko hayo pia yanaashiria kukubali kushindwa.

Kipigo walichokipata wapinzani kilichotokana na utambulisho wa kishindo ulioambatana na umati wa wananchi waliojitokeza kumuunga mkono mgombea huyo wa CCM, Abeid Amani Karume alipokwenda Tume ya Uchaguzi kuchukua fomu za kugombea Urais kilitosha kubainisha kukubalika kwake kwa umma.

Umati huo wa watu ulitoa taswira kamili ya CUF kushindwa kwani pamoja na wapinzani kwa muda mrefu kujilabu kwamba wanaungwa mkono na wananchi wengi, siku hiyo ilionekana wazi kuwa mawazo hayo yaliyokuwa ni kinyume chake.

Katika harakati za kutambulishwa wagombea wa CCM baada ya kuteuliwa na chama chao viongozi wa kitaifa wa CUF walikuwa wa kwanza kutangaza kulalamikia utambulisho huo. Madai waliyoyatoa ni kuwa CCM imeanza kampeni kabla ya wakati huku viongozi hao wa upinzani wakisahau mikutano waliyokuwa wakiifanya katika kuwahamasisha wafuasi wao kujiandaa mithili ya wanasuburi kwenda vitani.

Viongozi hao wa CUF pamoja na kulalamika kuwa CCM imeanza kampeni kabla ya wakati, walikuwa wakitishwa na wimbi la wafuasi wake wakiwemo viongozi waandamizi na Wabunge wa chama hicho kujitoa na kujiunga na CCM. Matukio hayo ni dalili tosha zinazoashiria kushindwa kwa chama hicho.




Mbali na hali hiyo CUF, tayari imeshalalamika kuwa uchaguzi huenda usiwe huru na wa haki kwa sababu ya kutokuwa na imani na mchakato mzima wa kuandikisha wapiga kura.

Tamko la Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad la kubainisha kwamba hatokubali mmatokeo yoyote ya uchaguzi hata endapo yeye mwenyewe atashinda lilitosha kubainisha kulia uteka. Matamshi hayo ni sehemu ya kukata tama kabla ya hata uchaguzi haujafanyika.

Vigezo vyote hivyo vinaweka bayana kushindwa kwa CUF katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utakaofanyika Oktoba 30, 2005. Hali hiyo sasa inafahamika hata kwa baadhi ya wafuasi wa chama hicho na ndiyo iliyoshusha hamasa za wafuasi hao za kwenda kwa wingi katika mikutano ya hadhara imepungua sana hivi sasa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla.

CUF iliyozoea kushindwa na badala yake kudai kuwa wameibiwa kura kama ilivyofanya mwaka 1995 na 2000, tayari imeshaonesha dalili za kushindwa tena mara ya tatu mfululizo ambapo viongozi wa chama hicho wanaeleza wazo kuwa kuwa huenda mambo yakawa kama yalivyokuwa chaguzi ziliopita.

Kwa kufahamu hivyo, ndio maana chama hicho kikatoa tamko la kutaka kususia uchaguzi Zanizbar iwapo madai kilichotoa juu ya hitilafu kwenye daftari la kudumu la wapiga kura hazitapatiwa ufumbuzi kwa muda maalumu uliotolewa ambao umeshamalizika.

Kinachodhihirika ni kubainika wazi kwamba upinzani umeshashindwa hata kabla ya kupigwa kura. Na kinachoshindilia msumari wa mwisho katika jeneza hilo la CUF ni kujitokeza kwa wingi wafuasi wa CCM kwenye mikutano ya kampeni ya CCM. Wingi huo unaifanya CCM kuendelea kuzoa kura katika uchaguzi ujao na dalili tosha ya ushindi wa kishindo.

No comments: