Monday, July 9, 2007

JIWE MOJA KWA NDEGE WAWILI

SHEREHE ZA KUTIMIA MIAKA 29 YA KUZALIWA KWA CCM NA USHINDI WA CCM KUTIMIA MWAKA MMOJA
“Tunasherehekea Chama chetu cha Mapinduzi Kuuwa Ndege Wawili kwa Jiwe moja….. Kwanza siku ya leo Februari 5 ya mwaka huu, Watanzania na hasa wana CCM tunasherehekea Chama chetu kimetimiza umri wa miaka 29 tangu kuzaliwa kwake hapo Februari 5, 1977. Pili Sherehe hizi zinakwenda sambamba na sherehe za ushindi mkubwa wa CCM kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Hayo ni baadhi tu ya maneno yaliyotamkwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zabnzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Amani Abeid Karume, wakati akihutubia wana CCM na wananchi wa Mikoa mitatu ya Unguja katika mkutano wa hadhara wa kilele cha maadhimisho ya miaka 29 ya CCM – Februari 5, mwaka huu, uliofanyika Pwani Mchhangani, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Amani Abeid Karume. Mwandishi wa Makala haya ALI ABDULRAHMAN NDOTA, aliyefuatilia kwa karibu sherehe hizo anaelezea zaidi……

KILA ifikapo Februari 5 ya kila mwaka , wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla, huwa wanasherehekea maadhimisho ya sherehe za kuzaliwa kwa Chama chao. Mbali ya kawaida ya miaka iliyopita, wanachama hao wamesherehekea maadhimisho ya mwaka huu kwa staili ya aina yake, kwani wameshuhudia Chama chao kikitimiza umri wa miaka 29 tangu kuzaliwa kwake mwaka 1977.

Hakika, miaka 29 ni muda mfupi sana kuweza kupima maendeleo ya jamii. Hata hivyo muda huo unatosha kabisa kupima shughuli za Chama cha Siasa kinachoongoza nchi kama CCM na mafanikio yake. Sina haja ya kuelezea maendeleo yaliyoletwa hapa nchini na Serikali za Chama Cha Mapinduzi, kwani yanafahamika na kueleweka na kila mwananchi wa Taifa hili. Lakini nitakuwa mwingi wa fadhila endapo sitagusia kitu kwa upande wa maendeleo yaliyosambazwa na yanayoendelea kusambazwa siku hadi siku anchini humu.

Tangu Chama cha Mapinduzi kizaliwe miaka takriban ishirini na tisa iliyopita, Watanzania wenye umri huo na wale wa zaidi ya umri huo, wamekuwa mashuhuda wa jinsi CCM ilivyopania kuleta maendeleo endelevu kwa maslahi ya wananchi wake. Kila uchao, Serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi, zimekuwa mstari wa mbele katika kuwaondelea kero mbali mbali zinazowagusa wananchi wa Mijiji na Vijijini.

Katika kipindi cha hivi karibuni, kumejitokeza watu au kikundi cha watu kinachojaribu kutoa kauli za kejeli eti Serikali za CCM zimefanya nini cha kimaendeleo katika kipindi chote hicho cha miaka 29. Ama kweli “mwenye macho haambiwi tazama”. Mathalan, Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Searikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanikiwa kufanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundo mbinu ya kiuchumi na ustawi wa jamii Mijijini na Vijijini. Lakini kubwa zaidi Serikali zote mbili za SMT na SMZ zimeweza kukusanya mapato kutoka vyanzio mbali mbali kwa kiasi kikubwa na pia zimefaulu kudhibiti matumizi mabaya (holela) ya mapato hayo. Aidha, zimefaulu kupunguza kama si kuziba kabisa mianya kadhaa iliyokuwa imeshamiri miongoni mwa wafanyakazi hasa wa shughuli za fedha nchini kote.

Hali hiyo imefikiwa baada ya Serikali hizo kuweka mikakati madhubuti ya kumiliki uchumi wa Tanzania usitumike kiholela ili kuwanyima nafasi wale wajanja wachache waliokuwa wakinufaika na mianya hiyo. Aidha, ongezeko hilo la mapato yanayokusanywa kwa kila mwezi, yameziwezesha Serikali za CCM kuweza kutoa ruzuku kwa vyama mbali mbali vya siaisa nchini ikiwemo Chama Tawala chenyewe (CCM).

Ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya wafuasi au viongozi wa vyama vya upinzani wakitoa kauli za udanyanyifu zenye lengo la kupotosha jamii kwa kusema “eti CCM inafuja mapesa mengi ya wavuja-jasho wa Taifa hili kwa kufanya sherehe zisizokuwa na mpango wowote”. Jibu la hoja hiyo ni kwamba Chama cha Mapinduzi kamwe hakitumii na wala hakitotumia fedha za Serikali zinazotokana na wavuja jasho katika kufanikisha mipango yake ya kimaendeleo na shughuli nyengine za kawaida. Fedha zinazotumika ni sehemu ya ruzuku yake ya kila mwezi inayopatikana kutoka Serikalini kama wanavyopata vyama vyengine vya siasa nchini.

Ni ukweli usio shaka kwamba Chama cha Mapinduzi kilianza rasmi sherehe za maadhimisho ya miaka 29 Januari 30 na kufikia kilele chake Februari 05, mwaka huu. Wana CCM walisherehekea maadhimisho hayo yaliyofanyika Ki-Mikoa kwa kufanya mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mashindano ya michezo ya kijadi, resi za ngalawa na baiskeli pamoja na Tamasha la Muziki - lililorindima katika Kumbi mbali mbali za Starehe Mijini na Vijijini. Hakika ufanisi wa mambo hayo yote hauwezi kupatikana bila ya kuwepo fedha za kutosha. Hivyo, ukweli wa mambo unabaki pale pale kwamba fedha zilizotumika zinatokana na ruzuku itokayo Serikalini mwezi hadi mwezi.

Katika maadhimisho hayo, Chama cha Mapinduzi kimeweza kuwaalika viongzi wa vyama vyote vya siasa nchini ili kushiriki kikamilifu kwa maadhimisho hayo. Kwa bahati nzuri, ni viongozi wa vyama viwili tu ndio waliohudhuria kwenye sherehe hizo ikiwemo na mkutano wa hadhara wa mikoa mitatu ya Unguja. Viongozi wa vyama vya NLD na DP, ndio pekee walioshiriki katika sherehe za miaka 29 ya kuzaliwa kwa CCM iliyokwenda sambasamba na sherehe za ushindi mkubwa mithili ya tsunami katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliopita. Chama cha Mapinduzi kinatoa mkono wa pongezi kwa vyama hivyo na kwamba ndio vyama vinavyojua umuhimu wa kuwepo kwa demokrasia ya vyama vingi nchini. Chama cha Mapinduzi ni Chama pekee kilichokomaa kisiasa, kitaendelea na juhudi ya kuvilea vyama hivyo vikiongozwa na CUF hadi pale vitakapoweza kujisaidia na kujua lipi zuri na baya kwa maslahi ya jamii nzima ya Watanzania.

CCM imeshinda kwa ushindi wa tsunami katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, lakini wafuasi wa CUF wakiongozwa na viongozi wao, wamekuwa mstari wa mbele kukejeli ushindi huo siku hadi siku. Ati ushindi huo umetokana na wizi wa kiini macho…. Mara ushindi huo unatokana na vibwengo…. Na madai mengine chungu nzima. Kama hiyo haitoshi, wafuasi hao (CUF) wameanzisha mtindo wa kupandisha bei ya vyakula pamoja na baidhaa nyengine muhimu madukani ikiwemo nguo, huku wakiitumia falsa ya CCM ya “Ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya” kama shahada inayowaruhusu wao kupandisha kiholela bei za bidhaa hizo.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Amani Abeid Karume, akiwahutubia mamia ya wana CCM na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 29 ya CCM huko Pwani Mchangani, aliliweka bayana suala hilo na kusema kwamba “wale wote wanaotumia falsa hiyo kwa kwenda kinyume na maana yake waache mara moja kufanya upuuzi huo”. Alidai Rais Karume.

No comments: